Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWATOA HOFU WAKULIMA WA PAMBA......WAZIRI MKUU ASEMA HADI JULAI 30 WAKULIMA WOTE WATAKUWA WAMELIPWA

Na Mwandishi Wetu

ZAO la pamba ni miongoni mwa mazao makuu ya biashara hapa nchini yakiwemo ya korosho, chai, tumbaku, katani na chikichi ambayo yamekuwa yakitegemewa katika kuinua uchumi wa wakulima na Taifa kwa ujumla.


Hivi karibuni kumetokea hali ya sintofahamu kuhusiana na suala ununuzi wa zao hilo baada ya kutangazwa kwa bei elekezi ambayo ni sh. 1,200 kwa kilo moja katika mikoa yote inayozalisha zao hilo.

Bei elekezi ya pamba kwa msimu huu ilitangazwa Aprili 30, 2019 mkoani Shinyanga na kwamba bei hiyo ilitakiwa ianze kutumika kuanzia Mei 2, 2019. Hata hivyo ununuzi wa zao hilo ulianza kwa suasua jambo ambalo Serikali haikuridhishwa nalo.

Jumapili ya Julai 14, mwaka huu ndipo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliamua kuitisha kikao kilichojumuisha wakuu wa mikoa 11 inayolima pamba, wanunuzi wa zao hilo, taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na Gavana wa Benki Kuu.

Kikao hicho kilichoitishwa na Waziri Mkuu na kufanyika katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi kilikuwa na lengo la kutafakari mwenendo wa zao la pamba ambalo ununuzi wake unaendelea lakini kwa kasi ndogo.

Waziri Mkuu baada ya kusikiliza changamoto za wanunuzi ambao wengi wao waliomba Serikali iwadhamini katika taasisi mbalimbali za fedha walizoomba mikopo kwa ajili ya kununua zao hilo kwa kuwa ilikuwa imekwama. Serikali iliwakubalia.

“Sasa tumefikia muafaka wa jambo hili kibali kitatoka na wote watakaopata dhamana ya mikopo hakikisheni fedha hizo zinaenda kutumia kwa ajili ya ununuzi wa pamba kama ilivyokusudiwa na si vininevyo.”

Hivyo, Waziri Mkuu aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya katika maeneo yote yanayolima pamba wawasimamie ipasavyo wanunuzi wote ili kuhakikisha fedha zitakazopatikana zinakwenda kutumika kwa ajili ya kununulia pamba.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi Binafsi wa Pamba (TCA), Bw. Christopher Gachuma aliishukuru Serikali kwa kukubali kuwadhamini pamoja na Waziri Mkuu kwa maelekezo aliyoyatoa kuhusu suala la ununuzi wa zao hilo.

Waziri Mkuu, baada ya kufanya kikao na wadau wa pamba wakiwemo na wanunuzi ambao walikubali kwenda kununua pamba iliyoko kwa wakulima, Julai 15, 2019 alifanya ziara katika wilaya ya Igunga kwa lengo la kukagua mwenendo wa ununuzi wa zao la pamba.

Akiwa katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alianza kwa kukagua ghala la ununuzi wa pamba la AMCOS ya Mbutu na kisha alikwenda katika kijiji cha Mwabakina na kukagua ghala la kununulia pamba la Mwabakima.

Baada ya kukagua maghala hayo Waziri Mkuu alizungumza na wananchi wa maeneo hayo ambao wengi wao ni wakulima wa pamba ambapo aliwahakikishia kwamba hadi kufikia tarehe 30 mwezi Julai mwaka huu pamba yote iliyoko katika mikoa mbalimbali nchini itakuwa imeshanunuliwa na wakulima wote kulipwa fedha zao.

Alisema Serikali imeamua kuingilia kati suala la ununuzi wa zao la pamba kutokana na kusuasua kwa soko lake kwa kutoa dhamana ili kuwawezesha wanunuzi kukopeshwa fedha na benki mbalimbali kwa ajili ya kununulia pamba kutoka kwa wakulima.


“Tunatambua adha mliyoipata tangu kuanza kwa msimu wa mwaka huu na hayo ni mapito tu. Nawasihi muwe na amani kwani Serikali yenu inafuatilia suala hili na Rais Dkt. John Magufuli anataka kuona pamba yote inatoka kwa wakulima ili kuwawezesha kupata tija.”

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwasihi wakulima wa zao hilo la pamba na wakulima wa mazao mengine nchini wahakikishe mara baada ya kuuza mazao yao wanatenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kununulia pembejeo watakazozitumia katika msimu ujao.

Wananchi kwa upande wao waliishukuru Serikali kwa hatua yake ya kuingilia kati suala la ununuzi wa zao la pamba pamoja na malipo kwa wakulima ambao tayari pamba yao walishaipeleka katika AMCOS zao.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga alisema Serikali itahakikisha inaendelea kutafuta masoko ya mazao hayo ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha wakulima kuwa na uhakika wa masoko kwa mazao yao na hivyo kujiongezea tija.

Pia, Waziri huyo alisema mbali na kutafuta masoko, Serikali imedhamiria kufufua viwanda mbalimbali vya nguo hapa nchini ili kuwawezesha wakulima wa zao la pamba kuwa na soko la uhakika. “Kuhusu suala la maghala tunatambua tatizo hilo na tutahakikisha tunayaboresha ili pamba iweze kuhifadhiwa katika mazingira bora”.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya viuatilifu, Waziri Hasunga alisema Serikali itahakikisha vinapatikana kwa kuzingatia eneo husika ili kuweza kudhibiti wadudu waharibufu.

(MWISHO)


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com