Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Taasisi ya kuzuia na kupambana Rushwa ,TAKUKURU kwa Mkoa wa Dodoma inawashikilia watu wawili akiwemo mtendaji wa kata kwa kosa la kupokea hongo ya Tsh.Milioni nne.
Akizungumza na waandishi wa habari Leo Julai 24,2019 jijini Dodoma mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Bw.Sosthenes Kibwengo amesema mtendaji wa kata ya Mlowa Bwawani wilaya ya Chamwino Bw. Luis Charles Pearson na Mgambo Bw.Josephat Ernest Msambili wote wenye umri wa miaka [37] walishikiliwa na TAKUKURU Kwa kosa la kushawishi na kupokea hongo ya Tsh.Mil.4 kinyume na kifungu cha 15[1]a cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa Na.11 Ya mwaka 2007.
Watuhumiwa hao walimkamata na kumweka mahabusu ya kata Bw.Samwel Mabway CHILULUMO ,mkazi wa kijiji cha WILIKO kilichopo kata ya MLOWA BWAWANI Kutokana na ugomvi wa kifamilia .
Wakati Chilulumo akiwa yupo Mahabusu ndipo watuhumiwa walipomtaka awape rushwa ya Tsh. Laki 6 ili wamwachie huru.
Hata hivyo ,Bw.Chilulumo aliomba kupunguziwa hadi kufikia Tsh.Laki nne na alipoomba atolewe mahabusu ili akatafute fedha hizo watuhumiwa walikataa na kuamua kwenda kumtafuta mteja wa mbuzi kumi[10] za Bw.Chilulumo zilizokuwa nyumbani kwake.
Aidha,Bw.Kibwengo amesema uchunguzi wa TAKUKURU umethibitisha kuwa Mtuhumiwa Bw.Msambili alikwenda kutafuta mnunuzi wa Mbuzi hao na kumpeleka Mahabusu alipokuwemo Bw.Chilulumo na baadaye kwenda nyumbani kuwakagua na akarudi tena mahabusu ndipo walipokubaliana bei.
Imethibitika kuwa mnunuzi huyo alitoa fedha hizo ambazo watuhumiwa walizipokea ndipo wakamtoa mahabusu na kumwachia huru na TAKUKURU imekamilisha uchunguzi wa suala hilo na watuhumiwa wamefikishwa mahakamani leo .
Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma ametoa wito kwa watendaji wa kata,mitaa,vijiji kuenenda kulingana na maadili ya Kazi zao na kujiepusha na vitendo vya Rushwa kwani havina nafasi katika serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli.
Social Plugin