Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAKUKURU YAWAPA ONYO KALI VIONGOZI WA UMMA 'WAPIGA DILI' SHINYANGA


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga imetoa onyo kali kwa viongozi wa umma wanaotumia utaratibu wa kutumia rasilimali za ndani 'Force Account' kujinufaisha wenyewe kwa kukiuka taratibu za manunuzi ya umma katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Onyo hilo limetolewa leo Julai 11,2019 na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga,Hussein Mussa wakati akizungumza na waandishi wa habari akielezea utekelezaji wa moja ya majukumu ya TAKUKURU mkoa huo kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2019 la kufuatilia fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Alisema baada ya TAKUKURU kufuatilia manunuzi ya vifaa yanayofanywa kwa kutumia 'Force Account' imebaini kuwa kuna baadhi ya manunuzi yanayofanyika yana kasoro mbalimbali kinyume na kusudio la serikali.

Hussein alisema wamebaini kuwa baadhi ya watumishi wa umma au wataalamu ambao huwa sehemu ya kamati za ujenzi au washauri wa ujenzi wanatumia nafasi zao vibaya kwa kutoa maelekezo ya ununuzi wa vifaa sehemu ambazo wana maslahi yao binafsi.

"Tumebaini kuwa manunuzi hufanyika kwa bei ya juu kuliko bei iliyopo sokoni lakini pia baadhi ya watumishi wa umma wanaohusika kufanya manunuzi hujaza wao wenyewe hati msako hivyo kupelekea kujaza hadi kampuni au jina la biashara hewa ilmradi kampuni au mfanyabiashara anayekusudia apate kazi na kuna utaratibu wa utunzaji nyaraka za utekelezaji miradi hauridhishi",ameeleza Mussa.

"Viongozi hawa wanafanya malipo makubwa ya matumizi ya vifaa tofauti na uhalisia wa vifaa wanavyopokea na kamati za ujenzi zinazoundwa hazifanyi ushindani halisi wa bei za vifaa badala yake wanapanga bei kwa kumpa mfanyabiashara mmoja kujaza hati msako zote na kupanga bei bei wanayotaka hivyo kuiingizia serikali hasara",aliongeza.

Mkuu huyo wa TAKUKURU aliitaja miradi iliyotembelewa na TAKUKURU kuwa ni elimu,afya,maji,miundombinu na nishati na kwamba mpaka sasa wameanzisha uchunguzi katika miradi minne yenye thamani ya shilingi 644,864,180/= na ushahidi wa kutosha ukipatikana watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Hata hivyo alizitaja idara zinazoongozwa kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa kuwa serikali za mitaa,polisi,mahakama,ushirika,elimu,sekta binafsi,maji,madini,misitu,mawasiliano,afya,ardhi na ujenzi.

Na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com