TAKUKURU YAKAMATA TAPELI SUGU ANAYEJIFANYA AFISA WA USALAMA WA TAIFA-IKULU NA KUTAKA KUMTAPELI MKUU WA WILAYA

Ndugu Waandishi wa Habari,

Awali ya yote kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na watumishi wote, napenda mpokee salamu zetu za POLE kwa msiba mkubwa ambao umewapata waandishi wenzenu kutoka Azam Media Limited.

Vilevile, nachukua fursa hii kuwashukuru Waandishi wa Habari kwa ushirikiano ambao mmekuwa mkiutoa kwa TAKUKURU kila tunapowaalika ili kuzungumza nanyi.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Tumewaita leo ili kuutarifu umma kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ofisi ya Dar Es Salaam, inamshikilia mtu mmoja mkazi wa Chamazi Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma za kujifanya Afisa wa Serikali – kutoka ofisi ya USALAMA WA TAIFA.

Mtuhumiwa huyo anayejulikana kwa jina la Omari Khamis Chuma mwenye umri wa miaka 55, alikamatwa na Maafisa wa TAKUKURU baada ya TAKUKURU kupokea taarifa kuwa mtuhumiwa huyo alifika katika Ofisi za Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Bi Jokate Mwegelo kwa nia ya kumtapeli kwa kujifanya kuwa yeye ni Afisa wa Serikali kutoka Usalama wa Taifa – IKULU.

Baada ya kupokea taarifa hizi pamoja na taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali, TAKUKURU ilianzisha uchunguzi dhidi ya mtuhumiwa huyu na kuthibitisha makosa chini ya sheria zifuatazo ikiwemo Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007:

i. Kujifanya Afisa wa Serikali kinyume na kifungu Na 100 (b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code) Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002
ii. Kuomba, kushawishi au kujaribu kujipatia au kujipatia rushwa kinyume na Kifungu Na. 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11/2007

Hatua ya kumkamata TAPELI huyu imefikiwa takriban wiki tatu tu tangu TAKUKURU iutangazie umma juu ya kukamatwa kwa MATAPELI wengine 6 waliokuwa wakishirikiana kufanya UTAPELI. Kati ya watuhumiwa wale – Wanne (4) kati yao walijifanya kuwa ni MAAFISA WA TAKUKURU pamoja na maafisa wa Vyombo vingine vya Dola na wawili kati yao walitoka katika makampuni ya Simu.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Uchunguzi wetu umebaini kuwa MATAPELI hawa wana mtandao unaojumuisha watu kutoka maeneo na ofisi mbalimbali zikiwemo za Serikali na wamekuwa wakiwafuatilia watumishi au viongozi ambao kwa njia moja au nyingine wanaweza kuwa na tuhuma na hivyo kuwadai fedha (RUSHWA) huku wakijifanya wao ni Maafisa kutoka TAKUKURU au USALAMA WA TAIFA.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa mara nyingine tena TUNATOA AGIZO KUPITIA VYOMBO HIVI VYA HABARI KUWATAKA MATAPELI HAO KUACHA MCHEZO HUU MARA MOJA KWANI TAKUKURU IKO MACHO NA INAYO MAMLAKA KISHERIA YA KUWACHUKULIA HATUA WALE WOTE WANAOJIHUSISHA NA VITENDO VYA UTAPELI.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa kuwa mtuhumiwa huyu alitenda makosa haya katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, basi atafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi - Mkoa wa Pwani leo Jumatano Julai 10, 2019 ili kujibu mashitaka yanayomkabili.

Tunaendelea kutoa tahadhari kwa jamii na kuwataka kuwa makini na KUTOKUBALI kurubuniwa kwa njia hizi wanazozitumia MATAPELI wa aina hii kujinufaisha.

Vilevile, tunaendelea kuwahimiza wananchi kutupatia taarifa sahihi za MATAPELI wa aina hii au yeyote anayejihusisha na vitendo vya Rushwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa bila kumwonea mtu au kumpendelea yeyote.

Taarifa hizi zinaweza kutumwa kwetu kupitia mfumo rasmi wa mawasiliano lakini pia wanaweza kuwatumia Viongozi wa Dini au chombo chochote cha Dola na taarifa hizo zitatufikia.

Tunatoa shukrani kwa wananchi ambao wamekuwa ni msaada mkubwa katika kutupatia taarifa ikiwa ni pamoja na wadau mbalimbali tunaoshirikiana nao katika kueneza elimu dhidi ya rushwa kwa jamii yetu.

IMETOLEWA NA:

ALI S. MFURU
KAIMU MKURUGENZI WA UCHUNGUZI
TAKUKURU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post