Na Emanuel Mayunga - Malunde1 blog Sumbawanga.
Viongozi wa kimila mkoani Rukwa wametoa tamko kali kulaani vikali taarifa mbalimbali zinazoendelea kutolewa kuuchafua Mkoa wa Rukwa pamoja na mambo mbalimbali yanayolenga kukwamisha juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Wakitoa tamko hilo mara baada ya matambiko yao kukamili yaliyofanyika Jumatatu wiki hii katika Mlima wa Itwelele uliopo katika kijiji cha Milanzi Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, machifu hao wa kabila la Kifipa wakiongozwa na mwenyekiti wao Chifu Kutazunga Mambwe Sisampa Sichula wa himaya ya Mambwe wamelaani vikali taarifa zinazotolewa ambazo zinalenga kuutangazia sifa mbaya mkoa wa Rukwa kinyume na hali ilivyo na asili ya wakazi wa Mkoa huo.
Machifu hao wamesema kuwa mkoa wa Rukwa umekuwa ukitangazwa kushika nafasi ya mwisho kwa umaskini, mimba za utotoni na magonjwa ya utapiamlo kwa watoto wadogo hali ambayo inarudisha nyuma juhudi za maendeleo kwa wanarukwa na kuaminisha mambo yasiyofaa katika mkoa.
“Mkoa wa Rukwa ni moja ya mikoa michache nchini yenye fursa na rasilimali nyingi zikiwemo utalii kupitia vivutio vya ndani ya mkoa, shughuli za uvuvi kupitia ziwa Rukwa na ziwa Tanganyika, uzalishaji mkubwa wa kilimo ,licha ya hayo yote bado mkoa wetu umesahaulika sana katika masuala ya masoko ya mazao ya mahindi yanayolimwa kwa wingi pamoja na soko la Samaki sasa unaposema mkoa wa Rukwa unaongoza kwa umaskini ni kutaka kutudhalilisha” alisema Chifu Chilingo Katata, Mwene wa himaya ya Milanzi.
Aidha machifu hao wamekemea vikali tabia ya baadhi ya vijana wanaowarubuni wanafunzi kwa kuhusiana nao kimaenzi, kuwapa ujauzito na kukwamisha masomo yao wakiwataka waache mara moja tabia hiyo na kwa kijana yeyote atakayebainika amesababisha adha hiyo basi ajiandae kuhamishiwa mimba hiyo.
"Mkoa wa Rukwa tumekuwa tukiripotiwa kwa mimba za utotoni na wanafunzi kufupisha masomo yao kwa sababu mbalimbali zikiwemo ujauzito, kwa kijana yeyote atakayebainika kumpa ujauzito mwanafunzi yeyote katika mkoa wa Rukwa machifu tumekubaliana kuwa ujauzito huo tutamhamishia kijana mhusika ili iwe fundisho kwa vijana wengine wenye tabia mbovu zinazochafua mkoa wetu",alisema.
Akipokea tamko la machifu hao na kuahidi kulifikisha sehemu husika, mkuu mkoa wa Rukwa ndugu Joachim Wangabo amewapongeza machifu hao kwa tamko lao na kusema kuwa wameonesha uzalendo mkubwa kwa mkoa wa Rukwa na ustawi wa taifa la Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Wangabo aliongeza kuwa tamko hilo la machifu mkoa wa Rukwa limekuja muda muafaka ukilinganisha na mambo mbalimbali yanayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini yanayosababishwa na baadhi ya watu wanaojaribu kukwamisha juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais Magufuli kwa kushirikiana na watendaji wake na hivyo itasaidia kuonesha msimamo na mshikamano madhubuti wa kutambua maendeleo na kushiriki kila mmoja kwa nafasi yake na badala ya kuharibu ustawi wa Taifa.
Aidha mkuu wa mkoa amewaasa viongozi hao wa jadi kuunga mkono juhudi za Rais kwa vitendo na kusaidia kukemee mmomonyoko wa maadili kwa jamii na kusaidia kukomesha tabia zisizofaa zikiwemo za ujauzito kwa wanafunzi mashuleni.
chifu malema Richard Sinyangwe wa himaya ya nkasi machifu wakifanya Tambiko katika pango la Itwelele
Mwene Malema Richard Sinyangwe wa himaya ya Nkasi akikabidhi tamko kwa niaba ya machifu wenzake kwa Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo.
Machifu na wazee wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ndugu Joachim Wangabo baada ya kumkabidhi tamko lao
****
TAMKO LA MACHIFU WA KABILA LA WAFIPA NA WAZEE WASHAURI WA MACHIFU WA
MKOA WA RUKWA LA KUPONGEZA NA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA MH. DKT. JOHN JOSEPH POMBE MAGUFULI KATIKA
KUWALETEA WATANZANIA MAENDELEO YA KWELI
Sisi Machifu wa kabila la wafipa kwa ujumla wetu, tukishirikiana na wazee wa Mkoa
tunapongeza juhudi unazozifanya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt.
John Joseph Pombe Magufuli katika kufanya mageuzi makubwa kwenye nyanja mbalimbali za
mfumo wa maisha (usawa,maadili,uzalendo n.k) na kuleta maendeleo ya kweli kwa
Watanzania. Tumeshuhudia mambo makubwa mno yakifanyika katika Taifa letu ambayo
hayakuwahi kutokea wala kutegemewa ndani ya kipindi cha miaka mitatu na miezi michache
ya utawala wako adhimu na wa kizalendo.
Miongoni mwa baadhi ya mambo makubwa ya kimaendeleo yaliyofanyika Kitaifa ni pamoja na:-
1. KUREJESHA HESHIMA NDANI YA UTUMISHI WA UMMA.
Uteuzi makini wa viongozi mbalimbali wa Wizara, Mikoa, Wilaya na Halmashauri zote
pamoja na usimamizi wa karibu, umerejesha na kuongeza nidhamu ya uwajibikaji pamoja
na uadilifu katika Taifa letu. Hii pia imeongeza heshima ya kazi na kuboresha mahusiano ya
wahudumu katika Idara mbalimbali serikalini na wahudumiwa hasa wanyonge.
2. KUTAMBUA UWEPO WA TAWALA ZA JADI KITAIFA NA UTAMADUNI WA MTANZANIA
KUPITIA WIZARA HUSIKA
Sisi Machifu tunaona fahari kubwa sana kuwa na Rais anayeheshimu wazee na viongozi wa
mila, kwani kwa kufanya hivyo tumekuwa kiungo bora kati ya wazee, vijana, wanawake,
walemavu pamoja na watoto. Hii imerahisisha ushirikishwaji wa makundi yote katika
shughuuli mbalimbali za kimaendeleo kwa ujumla na utii kuongezeka katika jamii hapa nchini.
Aidha tunatoa pongezi za dhati kwa uongozi wa serikali ya awamu ya tano kwa kupambana na
rushwa ,matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana,umomonyoko wa maadili kijamii wazee kwa
vijana,ufisadi,kupotea kwa uzalendo kwa nchi na rasilimali za taifa.
3. KUPAMBANA KWA VITENDO NA KWA DHATI DHIDI YA RUSHWA, UFISADI NA
UBADHILIFU WA MALI ZA UMMA NA RASILIMALI ZA NCHI YETU KWA KUANZISHA
MAHAKAMA YA MAFISADI NA KUFUTA NA KUFUMUA BAADHI YA MIKATABA.
Wala rushwa na wabadhilifu wa mali za Umma, walikuwa ni viongozi wakubwa waliolitumikia
Taifa letu kwa muda mrefu, wakishirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu ndani na nje
ya Taifa letu. Kuhujumu miradi mbalimbali ya Kitaifa. Hujuma hizo ziliongeza mzigo katika
uendeshaji wa Serikali na katika harakati za maendeleo. Miradi mbalimbali ilikuwa haiendi sawa kutokana na wenye mamlaka kuwa na urasimu mwingi katika kutengeneza mazingira na
mianya ya rushwa na hivyo miradi kunufaisha wachache badala ya kunufaishaTaifa kwa
ujumla.Aidha tumeshuhudia mikataba kadhaa ikifumuliwa au kufutwa ili kunufaisha
watanzania. Tunakupongeza sana kwa juhudi hizi ulizozifanya hata kama Watanzania
wengine wachache wanaumizwa na hatua hizi.
4. UJENZI WA MIRADI MBALIMBALI MIKUBWA YA KIHISTORIA
Mheshimiwa Rais,kwa kutumia serikali yako makini,umethubutu kujenga miradi mikubwa
mno, ambayo ni moyo wa maendeleo ya kweli kiuchumi kwa Taifa letu. Miradi hiyo ni Reli ya
Kisasa (Standard Gauge Rail), kituo kikubwa cha kufua umeme (wa mega wati Zaidi ya 2000)
katika bonde la mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Hydro-Electrical power project), ujenzi wa barabara
za juu DSM (fly overs)kupunguza foleni pamoja na barabara nyingine muhimu katika nchi
nzima, ujenzi wa meli kubwa, upanuzi wa bandari mbalimbali, ujenzi wa bomba la mafuta
Tanga-Oyma Uganda,ujenzi wa ukuta wa Mererani Arusha kulinda madini adimu duniani ya
Tanzanite na uanzishaji wa masoko ya madini kila mkoa nchi nzima, upanuzi na ujenzi wa
Hospitali za Mikoa, Wilaya, vituo mbalimbali vya Afya pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya
kisasa, ufufuaji wa shirika la ndege, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege mpya n.k.
5. KUFANIKISHA UHAMISHAJI RASMI WA MAKAO MAKUU YA NCHI KUTOKA DAR ES
SALAAM KWENDA DODOMA, NA KUTANGAZA DODOMA KUWA JIJI LA KISERIKALI.
Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli umekuwa Jemedali hodari uliyethubutu na umeweza
kuhamisha makao makuu ya nchi kwenda Dodoma licha ya makundi ya watu waoga
kukupinga.Pia tunakupongeza kwa kupandisha hadhi mji wa Dodoma kuwa Jiji na kufanikiwa
kuwashawishi wadau na marafiki wema wa nchi yetu kuamua kutoa ufadhili wa kujenga
uwanja mkubwa zaidi wa mpira wa miguu na michezo mingine ndani yake.
6. KUSIMAMIA KIKAMILIFU NA KWA UADILIFU MKUBWA RASILIMALI ZA TAIFA LETU
Kulikuwa na hujuma kubwa katika rasilimlai nyingi za Taifa letu. Madini, wanyama pori, misitu,
mafuta, gesi, samaki pamoja na rasilimali nyingine viliibwa na wawekezaji wasio waaminifu
wakishirikana na baadhi ya watanzania wenzetu wasioitakia mema nchi yetu. Mh. Dkt. John
Joseph Pombe Magufuli umeweza kudhibiti haya yote; Sisi kama Machifu hatuwezi kukaa
kimya bila kukupongeza na kukuunga mkono kwa mambo makubwa na mazuri kwa Taifa
uliyoyafanya.
7. KURUDISHA HESHIMA YA NCHI KWA KUTOKWENDA NJE YA NCHI KUOMBAOMBA NA
KUTETEA UTAMADUNI WETU.
Mh. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ulitangaza kwamba hautakwenda nchi za nje hasa
Ulaya kuombaomba misaada kwa sababu misaada hiyo ilikuwa na masharti fedheheshi kama vile kukubali ndoa za jinsia moja, utoaji mimba, ushoga, usagaji na mengine mengi yaliyo
kinyume na utamaduni wetu. Kutangaza kwamba haya siyo maadili ya Kitanzania, sisi machifu
tumefarijika sana na kuona kwamba heshima ya Waafrika Watanzania na Wafipa tukiwemo
imelindwa na kiongozi shupavu asiyeogopa kitu. Mh. Rais umekuwa mfano wa kuigwa na
kivutio cha wengi duniani kwa jinsi unavyopambana na magumu ili kulivusha Taifa letu
kuelekea uchumi wa viwanda. Kwa pamoja machifu tunakupongeza na kukuunga mkono kwa
asilimia 100%.
8. KAMPENI KUBWA YA KUPAMBANA NA MADAWA YA KULEVYA PAMOJA NA UHARIBIFU
WA MAZINGIRA NA KUTANGAZA SIKU YA USAFI KITAIFA.
Mh. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, umekuwa mkombozi wa kweli kwa vijana, wazee na
wanawake wa Tanzania waliokuwa waathirika wa biashara hizo. Yapo madhara makubwa, kwa
Taifa yatokanayo na matumizi na biashara ya madawa haya ya kulevya. Madhara hayo ni
pamoja na kiafya, kijamii, kiutamaduni, kiusalama na pia kuongeza umaskini kwa kasi katika
familia na jamii ya watanzania. Kitendo cha kudhibiti biashara hizi, Taifa linajihakikishia uwepo
wa nguvu kazi ya kutosha,usalama wa kiafya kwa jamii, kuimarika kwa ulinzi na usalama wa
Taifa letu, pamoja na kupungua kwa mizigo ya makundi tegemezi nchini. Tunakupongeza na
kukuombea uendeleee kwa kasi ileile katika kudhibiti utunzaji wa mazingira na katika hili
ingefaa upitishwe utaratibu/sheria kulazimisha kila kaya kupanda miti ya asili nay a kibiashara
walau asilimia kumi ya kila ardhi inayomilikiwa na kaya husika; umepiga marufuku matumizi
ya mifuko ya plastiki na kudhibiti uchafu wa kemikali za migodini na viwandaji kupitia NEMC.
Hilo ni jambo kubwa linalostahili pongezi za dhati.
9. UTOAJI WA ELIMU BILA MALIPO KUANZIA DARASA LA AWALI HADI KIDATO CHA NNE NA
UTOAJI WA MIKOPO KWA WAKATI.
Serikali ya awamu ya tano ikiongozwa na Mh. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, ilianza kutoa
elimu bila malipo kuanzia mwaka 2016 januari. Idadi ya watoto wa Kitanzania waliopata elimu
imeongezeka. Pia bodi ya mikopo imekuwa makini kutoa mikopo kwa wakati na kuwawezesha
watoto wetu kusoma bila usumbufu. Jambo hili limepunguza na kumaliza kabasa migomo ya
wanafunzi wa vyuo vikuu iliyokuwa inaleta taswira mbaya duniani na kutia doa heshima na
ubora wa elimu kwa wahitimu wa elimu katika ngazi mbalimbali. Tunatoa pongezi za dhati na
mwenyenzi Mungu azidi kukupa afya ya roho na mwili.
10.KUTOA MIKOPO YENYE MASHARTI NAFUU KWA VIJANA WANAWAKE NA WALEMAVU
KUPITIA HALMASHAURI ZOTE NCHINI
Serikali yako ya awamu ya tano, umethubutu kuwapa mikopo wananchi wako asilimia 10%
yamakusanyo ya mapato ya halmashauri husika ili zitumike katika kujenga uchumi wa
wananchi wa kipato cha chini. Fedha hizi hazina riba wala dhamana. Hii imesaidia wanawake,
vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi endelevu wa Taifa
letu. Yapo mambo mengi yaliyofanywa kwa ufanisi na Serikali hii makini. Tumepata umeme
wa REA, huduma ya maji safi na salama kwa kila Halmashauri. Huduma ya Afya ya wafungwa,
mahabusu pamoja na makundi mengine muhimu katika Taifa letu. Yote haya yanatugusa na
kutufanya tukupongeze kwa dhati. Tunaamini wewe ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Endelea kulifaa Taifa letu kwa yote mema unayofanya na sisi tuko pamoja na wewe katika
hatua na namna zote na kwa yote mengi mema.
Mh. Rais kiukweli umefanya mambo mengi mazuri pia katika Mkoa wetu wa
Rukwa.Miongoni mwa mambo hayo ni:
-
1. Ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wetu. Serikali ya awamu ya tano
inajenga chuo kikubwa nacha kisasa cha VETA Kashai- Manispaa ya Sumbawanga, Daraja la
mto Momba ambalo ni daraja kubwa na refu kupita madaraja yote ya Mkoa wetu wa
Rukwa,Daraja la Kirando kwenda Utinta, Ujenzi wa vituo vya Afya, hospitali za Wilaya na
ukarabati wa hospitali ya Mkoa pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, upanuzi wa
uwanja wa ndege wa Sumbawanga ambao tayari wananchi wameshalipwa fidia kupisha
upanuzi,Uhamishaji wa chuo cha ualimu Sumbawanga kutoka Kantalamba kwenda kijiji cha
Pito ambapo tayari wananchi wameshalipwa kupisha ujenzi kwenye ardhi husika,ukarabati
wa shule ya Sekondari Kantalamba,pamoja na ukamilishaji wa uwepo wa chuo kikuu cha
MUST tawi la Rukwa kilichopo Kianda.
2. Miradi mingine mikubwa ni ujenzi wa barabara za lami ndani ya Manispaa ya Sumbawanga,
ujenzi wa stendi kubwa na ya kisasa Katumba Azimio na miradi mikubwa ya maji katika
halmashauri zetu zote zilizopo ndani ya Mkoa.
3. Usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa REA, Mkoa wetu umenufaika sana na
umeme huu. Tunatoa shukrani na pongezi za dhati kwako Mh. Rais.
4. KUTULETEA VIONGOZI MAKINI NA WAZALENDO WA KWELI NDANI YA MKOA WETU.
Sisi machifu na wazee wa mkoa tunakushukuru kwa kuteua na kutuletea viongozi wasaidizi
wakomakini wa kuteuliwa wanao chapa kazi wakishirikiana vema na tawala za jadi zilizopo
katika mkoa wetu. Viongozi hawa ni Mkuu wa Mkoa, katibu tawala Mkoa, wakuu wa
Wilaya, makatibu tawala wilaya,wakurugenzi pamoja na watendaji wengine wapya kupitia
awamu yako hii katika ngazi na idara mbalimbali. Hii imeimarisha ufanisi wa kazi katika kusukuma maendeleo ya mkoa wetu. Pia ushirikiano mkubwa wa Serikali ya mkoa na
viongozi wa jadi yaani machifu umeongeza ushiriki chanya wa wananchi katika kujiletea
maendeleo endelevu ya mkoa.
TAMKO;
Mhe. Rais, Mkoa wetu wa Rukwa, zamani ukijulikana kama” Ufipa District”, una historia
kubwa sana ya kushiriki katika ukombozi wa Taifa letu (Tanganyika) pamoja na kushiriki katika
mipango ya maendeleo. Baadhi ya matukio yanayobainisha na kutunza historia hiyo ni pamoja na:-
1. Kwamba, barua ya wito kwa Hayati baba wa Taifa Mwalimu J.K. Nyerere kwenda kwenye
mkutano wa umoja wa Mataifa UNO New York Marekani aliipokea UFIPA, kwenye mkutano
wa chama cha TANU katika kijiji cha Mpui.Barua hiyo Mwalimu aliipokea kupitia kwa
Dantesi Ngua ambaye alikuwa ni mtoto wa Mwene Maria (mdogo wa chifu Agustina NTI wa
wafipa Himaya ya Lyangalile) mwaka 1959. Barua hiyo ndiyo iliyopelekea Tanganyika
kupata madaraka ya kiserikali.
2. Vilevile Mwalimu Nyerere aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika akiwa
kwa rafiki yake marehemu Baba Askofu Msakila mzalendo wa kweli wa mkoa, ambaye
alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga ambayo ni nchi ya Ufipa.
3. Pia mwaka 1970 Mwalimu Nyerere alihamishia kwa muda wa Zaidi ya mwezi mmoja
Halmashauri kuu ya chama cha TANU na Baraza la Mawaziri katika kijiji cha Matai pale
kwenye chuo cha makatekista- Santa Maria ili kujadili,kujifunza na kuhamasisha juu ya
uanzishaji wa vijiji vya ujamaa. Mipango ya kuanzisha vijiji vya ujamaa na utekelezaji wake
ni baada ya chama na serikali nzima kuja kujifunza Ufipa District (MKoa wa Rukwa) kwa
kuwa Wananchi wa mkoa wa Rukwa walikuwa wakiishi katika vijiji vya ujamaa toka enzi,
kabla ya sera ya vijiji vya ujamaa na kupelekea serikali kumteua mwanarukwa Prof. Athanas
Kauzeni kuwa kamishna wa uanzishaji wa vijiji (villagelization) kitaifa na hadi leo kwenye
baadhi ya mikoa kuna majina ya vijiji vinaitwa “kijiji cha Kauzeni”.
4. Vilevile Wafipa ndio waliompa kwa mara ya kwanza Mwalimu Nyerere fimbo ya kwanza
kutumia yenye kichwa kikubwa kidogo kama ishara ya kumkubali na kumpa nguvu na
Baraka za kutawala nchi akiendelea na harakati za kutafuta uhuru wa Tanganyika. Baada ya
kutunukiwa heshima hiyo, mwalimu alifanikiwa na kuteuliwa kuwa waziri mkuu wa kwanza
wa Tanganyika akiwa katika nchi ya Ufipa, iliyoko mkoa wa Rukwa.
5. Tukio la kipekee pia kwa wafipa ni heshima tuliyopewa wakati wa kumzika mwalimu Julius
Kambarage Nyerere ambapo;
mwenyekiti wa Kamati ya mazishi Butiama aliteuliwa kuwa Mh. Paul Petro Kimiti Mfipa
mzaliwa wa Katapulo-Ulungu Rukwa.
Aliyeongoza gwalide la kijeshi katika kutoa heshima za mwisho kwenye mazishi hayo ni
Brigadia Generali Januari Chisanko ambaye ni Mfipa mzaliwa wa kijiji cha Mkima –Mpui
Lyangalile Rukwa,
Aliyeongoza ibada ya Misa takatifu ya mazishi ni Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo
ambaye naye ni mfipa mzaliwa wa kijiji cha Mwazye Himaya ya Mambwe Rukwa.
Kwa heshima tuliyonayo kwa Taifa hili tunaunganisha nguvu zetu na nia zetu zote na kutamka
kukupongeza Mh. Rais na serikali yako nzima kwa yote unayoendelea kuyafanya katika Taifa
letu kwa nia ya kutuletea wananchi wako maendeleo na kujenga taifa moja kwa kuimarisha
umoja, undugu, utulivu na mshikamano. Nasi kama watanzania tuweke kando itikadi za vyama
na dini zetu tuunge mkono nia njema ya Rais wetu.
Kwa Wanarukwa; Sisi Machifu wenu, tunakemea vikali mimba za utotoni mashuleni, kuanzia
leo, tabia hii ikome kwa wanaume wenye nia ovu la kuwakosesha watoto wa kike haki ya
kupata elimu, wazazi au walezi wenye watoto wa kiume chondechonde kemeeni na
kuwakanya vijana wenu, waache mara moja tabia hii, ili kuepuka adhabu kali ya kimila, Pia
tunaomba ushirikiano kwa wakuu wa shule na wakuu wa wilaya kutuhabarisha mtu
atakayesababisha mimba kwa mtoto wa shule, baada ya tamko hili, Pia tunaomba msaada kwa
Serikali za wilaya zetu zote, maafisa watendaji wa vijiji wapige mbiu kuwahabarisha wananchi
wao juu ya tamko hili, ili kusiwe visingizio pindi adhabu kali ya kimila itakapotolewa kwa mtu
wa aina hiyo.
Mwisho kabisa, tunakuomba mheshimiwa Rais uje Mkoani kwetu Rukwa (Ufipa Land), kwani
tuna mengi mno ya kuongea nawe kama machifu na wazee wazalendo wa mkoa wa Rukwa.
Tunakuhakikishia usalama wa kutosha wa kijadi, mara utakapoingia ndani ya Mkoa wetu wa
Rukwa, karibu sana, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Joseph
Pombe Magufuli.
Tunakutakia kila lililojema kwa Taifa letu na Watanzania kwa ujumla.
Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania, Mungu mbariki na kumlinda Rais wetu Mhe. Dkt.
Magufuli na wasaidizi wake wote serikalini. Mungu ibariki Rukwa yetu pamoja na wananchi
wote wa Tanzania.
Yote hapo juu, tumeyakabidhi kwa mizimu yote ya ardhi ya Ufipa, yaani ; Mizimu yote ya
himaya ya Milanzi, Ulungu, Iiwaa-Nkansi, Uwanda, Upimbwe, Mambwe, Lyangalile,
Sumbwanga Asilia, Iikwaa, MambweNkoswe na Uchile
Imeandaliwa na Machifu wote wa Mkoa wa Rukwa.
………………………………………….
Chifu Kutazunga Mambwe Sisampa Sichula
Himaya ya Mambwe
Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Rukwa.