Na Bakari Chijumba
Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba amesema Tanzania inakusudia kuwa mzalishaji mkubwa wa zao la korosho Duniani ambapo imeweka mkakati wa kufikia uzalishaji wa tani milioni moja ifikapo mwaka 2023/2024 kutoka tani laki tatu na kumi na tatu kwa sasa.
Akizungumza Ijumaa July 12, 2018 katika kongamano la kimataifa la uwekezaji kwenye sekta ya korosho lililoandaliwa na kituo cha uwekezaji nchini Tanzania (TIC) na kufanyika katika ukumbi wa Benki Kuu tawi la Mtwara, amesema vipo viwanda zaidi ya kumi ambavyo vimekuwepo tangu serikali ya awamu ya kwanza ambavyo teknolojia yake imepitwa na wakati na vingine havifanyi kazi kabisa.
“Mwalimu Nyerere mwaka 1978 hadi mwaka 1980 alijenga viwanda zaidi ya 12 ambavyo kwa sasa teknolojia yake imepitwa na wakati. Baadhi vimekufa na vilivyobaki vimepunguza uzalishaji,tumaeamua kuwaita wawekezaji ili kuviendeleza na kuanzisha vingine ili kuongeza uzalishaji” amesema Mgumba.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha uwekezaji nchini Tanzania (TIC) Geofrey Mwambe amesema Serikali imekuwa na matarajio makubwa ya kuwapo kwa ongezeko la uwekezaji katika zao la korosho ambapo wataanzisha viwanda kutokana na mwamko uliooneshwa na wawekezaji hao kwa kuwa wametambua fursa kwenye zao hilo.
Mwambe amesema wameamua kuandaa kongamoano hilo ili kushawishi wawekezaji wazawa na wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani ili wawekeze katika viwanda vya kubangua korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Pwani kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Tulitarajia kupata wageni 100 mpaka 150 lakini tumepata wawekezaji zaidi ya 300, Kwa idadi hii tumevuka lengo la kongamano letu na tunaimani watakuwa tayari kuwekeza kwenye viwanda vikiwemo viwanda vya korosho, nashukuru Wakuu wa Mikoa walioshiriki wote wametenga maeneo ya uwekezaji jambo ambalo linarahisisha kazi hii na kuifanya kuwa nyepesi" amesema Mwambe.
Mmoja ya wawekezaji kwenye kongamano hilo Mahamoud Sinani ameishukuru Serikali kwa kuwakutanisha pamoja na kuwawezesha kuzitambua fursa mbalimbali zilizopo katika kilimo cha zao korosho hapa nchini.
Social Plugin