Utawala wa rais Donald Trump unapanga kuanza utekelezaji wa operesheni ya nchi nzima inayolenga familia za wahamiaji, licha ya kupingwa vikali na Democrats.
Operesheni hiyo inasemekana kwamba inaweza kuanza kutekelezwa mwishoni mwa juma hili, baada ya kuahirishwa na Trump mwishoni mwa mwezi uliopita.
Inalenga kuwafuatilia watu walio na amri za mwisho za kurejea katika nchi zao, zikiwemo familia za wahamiaji ambazo kesi zao zilikuwa zikifutiliwa kwa haraka na majaji katika jumla ya miji 10 kama vile Chigaco, Los Angeles, New York na Miami.
Hatua hizo zimeibua hasira na wasiwasi miongoni mwa wanaharakati wa haki za wahamiaji na wabunge. Operesheni hiyo ni sawa na ile iliyowahi kufanywa mwaka 2003 na kisha kuwakamata watu wengi wasio na vibali.
Trump alitangaza kwenye Twitter mwezi uliopita kwamba operesheni hiyo itakuwa ni mwanzo wa kuwafukuza mamilioni ya watu wanaoishi Marekani kinyume cha sheria.