Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
SERIKALI kupitia Tume ya Madini imetoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini 350 katika mikoa ya Arusha na Katavi yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kutumia njia bora na za kisasa ili kuwawezesha kuachana na matumizi ya matumizi ya Zebaki yanayoathiri mazingira.
Akizungumza Alhamisi (Julai 4, 2019) katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere , Mkaguzi wa Madini na Mazingira wa Tume hiyo, John Mataro alisema Tume hiyo imekusudia kuhakikisha kuwa suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira linapewa na kila mchimbaji wa madini nchini.
Mataro alisema Ofisi hiyo imekuwa ikiotoa miongozo mbalimbali kupitia sheria zilizopo kwa ajili ya kuwaelimisha wachimbaji wadogo, na kampeni hiyo itakuwa endelevu ili kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayotumiwa na wachimbaji madini hususani wachimbaji wadogo yanazingatia maelezo hayo ili kuweza kuwa na uchimbaji endelevu na salama.
“Malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wachimbaji wetu wanaweza kupata kipato cha kutosha ili kuweza kujikwamua kiuchumi, na hili litafanyika kwa kuhakikisha kuwa tunajenga mazingira yenye usalama wa hali ya juu katkika maeneo yote ya uchimbaji yaliyopo nchini” alisema Mataro.
Aidha Mataro aliongeza kuwa Tume hiyo kwa kutambua mchango wa wachimbaji wadogo nchini imekuwa ikiwajengea uwezo wachimbaji hao kwa kujenga mazingira wezeshi ikiwemo kupata mikopo nafuu kupitia taasisi za kifedha ikiwemo Benki, hatua inayolenga kuwapa morali na uwezo wa kumiliki vifaa bora na vya kisasa kwa ajili ya uchimbaji wa madini.
Akifafanua zaidi Mataro alisema mara kwa mara Tume hiyo imekuwa ikifanya ziara katika migodi mbalimbali iliyopo nchini yenye lengo la kuwakumbusha wachimbaji wote hususani wachimbaji wadogo kuzingatia miongozo mbalimbali ikiwemo kuwepo matangazo mbalimbali ya tahadhari katika maeneo ya uchimbaji ili kuweza kutoa taarifa kwa wahusika wanaofika katika maeneo hayo kwa mara ya kwanza.
Social Plugin