Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UTURUKI YAANZA KUPOKEA MFUMO WA MAKOMBORA WA S-400 KUTOKA URUSI

Uturuki imepokea shehena ya kwanza ya mfumo wa makombora wa S-400 kutoka Urusi licha ya vitisho vya Marekani.

Uturuki ilipokea shehena hiyo katika uwanja wa ndege wa jeshi wa Murted jana Ijumaa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Ankara. 

Serikali ya Moscow imethibitisha habari hiyo ya kuanza kuikabidhi Uturuki mfumo huo na inasisitiza kwamba itaendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa makubaliano ya pande mbili.

Serikali ya Ankara imeanza kupokea mfumo huo wa makombora ya S-400 licha ya Rais Donald Trump wa Marekani kutahadharisha kuwa ataiwekea Ankara vikwazo vikali iwapo mfumo huo wa kujikinga na makombora wa S-400 kutoka Russia utawasili nchini Uturuki.

Mkataba wa mauzo ya ngao hiyo ya makombora kati ya Ankara na serikali ya Moscow ulitiwa saini Disemba mwaka 2017.

Jumatano iliyopita, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki alisema kuwa, iwapo nchi hiyo itashambuliwa na maadui, basi itatumia ngao hiyo ya makombora ya S-400 kujilinda.

Alisisitiza kuwa, Uturuki imeamua kununua ngao hiyo ya makombora kutoka Russia kwa ajili ya kujidhaminia usalama wake. 

Hata hivyo, maafisa wa Marekani hawataki kabisa ndege zao aina ya F-35 kuwa karibu na makombora ya S-400 - wakihofia wataalamu wa kirusi wataweza kung'amua mapungufu ya ndege hizo.

Marekani imeenda mbali kwa kutishia kuitoa Uturuki kwenye mpango wa kuendelea na manunuzi ya F-35 na kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi.

Uturuki hata hivyo inasema mifumo hiyo ya Urusi na Marekani itawekwa kwenye maeneo tofauti.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com