Taarifa kwa waandishi wa habari,
Ndugu Waandishi wa habari Chama cha Waandishi wa Habari wa Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania OJADACT kinalaani kitendo kilichofanywa na Msanii Irene Uwoya cha kudhihaki fedha yetu na kuwadhihaki Waandishi wa habari kwa kuwarushia fedha.
Msanii Irene Uwoya alionekana kupitia clip ya Video iliyosambaa akiwarushia fedha waandishi wa habari na baadhi ya waandishi waliokuwepo kwenye mkutano huo walipigana vikumbo kugombania fedha zilizorushwa na msanii huyo.
Tukio hilo lilitokea Julai 15:07:2019 Jijini Dar es Salaam wakati Irene Uwoya akizungumzia juu ya uzinduzi wa urushaji wa filamu kampuni ya swahili inflix.
Kitendo hicho ni kitendo cha dhihaka kwa waandishi wa habari na hakina sababu ya kufumbiwa macho zaidi ya kukemewa na kila mtanzania , kwani ni kitendo kinachobeba tafsiri ya dhihaka ndani yake na pia kwenda kinyume na sheria za Nchi. OJADACT, tunapiga Vita uhalifu huu kwetu ni uhalifu wa kuvunja sheria za nchi.
Kwa mujibu wa sheria ya benki ya Tanzania ya mwaka 2006, kifungu cha 26 benki kuu ndiyo yenye mamlaka juu ya fedha Nchini na sio Uwoya ambaye aliamua kudhihaki fedha kwa kuwarushia Waandishi wa habari.
Pia Sheria ya fedha inakataza mtu kudhihaki fedha, hivyo anapaswa akamatwe na ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria hizo.
Ndugu Waandishi wa habari mtambue kuwa, fedha ni moja ya alama ya Taifa, hivyo ni kosa la jinai kudhihaki na kukejeli sarafu au noti kama alivyofanya Msanii Uwoya kitendo hicho ni kwenda kinyume na sheria za nchi.
Yapo matukio ya nyuma yanayofanana na hili, mfano ni tukio la msanii Maua Sama ambaye alidhihaki fedha na kuchukuliwa hatua stahiki na vyombo vya Ulinzi na Usalama, Pia Benki kuu (BOT) ilitoa waraka wa kuwambusha watanzania kutodhihaki fedha kwani ni kinyume cha sheria.
Kwa upande wa waandishi nao waliyatupa pembeni maadili ya taaluma yao na kukubali kuidhalilisha taaluma ya habari kwa kujua wazi kuwa, kilichokuwa kinafanywa na Owoya sio sahihi, hivyo OJADACT tumesikitishwa na mwitiko wa Baadhi ya Waandishi hao na kuvunja maadili ya kitaaluma.
MAPENDEKEZO
· OJADACT tunaitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia kwa Waziri mwenye dhamana Harrison Mwakyembe kumchukulia hatua msanii Irene Uwoya mara moja ili iwe funzo kwa jamii.
· Wahariri wa vyombo vya habari husika vilivyotuma waandishi kwenye mkutano huo vifanye mapitio ya video iliyokuwa ikisambaa kuwabaini waandishi waliohusika na kuwapa onyo kali juu ya vitendo vyao vya kuidhalilisha taaluma ya habari
· Taasisi za kihabari ziongeze warsha za uchechemuzi kwenye vipengele vya maadili ya uwandishi wa habari
· Wadau wa habari wenye nia njema ya kufanya kazi na vyombo vya habari watoe mialiko kwa kutumia taasisi na sio mwandishi mmoja mmoja ili kusaidia kuthibiti utovu wa kimaadili kwa waandishi
· Wizara iwape mafunzo maalumu kundi la wasanii ili wazijue sheria za Nchi kwani inaonekana ni changamoto kwao kwenye kujua sheria.
WITO:
OJADACT tunatoa wito kwa Watanzania kuzijua sheria na kuzielewa ili kuepuka kuvunja sheria za Nchi.
Social Plugin