Kutokana na Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika mwezi ujao jijini Dar es Salaam, Wizara ya Viwanda na Biashara imeandaa Maonesho ya Viwanda kwa ukanda huo kati ya Agosti 5 hadi 9, yatakayofunguliwa na Rais John Magufuli.
Lengo la maonesho hayo yatakayofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) ni kuonesha bidhaa ambazo zinazalishwa na nchi wanachama.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa aliwataka wafanyabiashara na wenye viwanda nchini kujitokeza kutumia fursa hiyo kuonesha bidhaa zao ili kufungua milango ya kibiashara katika jumuiya hiyo.
“Katika kipindi hicho pia tutakuwa na Maonesho ya Viwanda ambayo yatafunguliwa na Rais na kufungwa Agosti 9 na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, lakini pia tunaandaa na chakula cha jioni,” alisema Waziri Bashungwa.
Alisema katika maonesho hayo viwanda zaidi ya 1,000 vinatarajiwa kushiriki, na mpaka sasa wafanyabiashara 580 wengi wao wakiwa watanzania wameshaomba kushiriki.
Alisema pia kuwa katika siku hizo kutakuwa na ziara ya kutembelea viwanda mbalimbali vya hapa nchini ili kuweza kujifunza.
Alisema ni heshima kubwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo mkubwa ambapo alimpongeza Rais Magufuli kuonesha nia ya dhati ya kujenga nchi ya viwanda jambo ambalo limezivutia nchi nyingine na kupenda kujifunza.
Aidha, Waziri Bashungwa alisema soko la SADC ni kubwa na lina fursa nyingi ambazo bado hazijatumiwa vizuri lakini kupitia mkutano huo pamoja na maonesho hayo watu watajifunza na kuweza kujua ni jinsi gani ya kufanya biashara ndani ya jumuiya hiyo.
Waziri huyo alisema hivi sasa wizara yake inapitia sheria, kanuni na miongozo ambayo inasababisha vikwazo katika biashara na kurekebisha ambapo alisema marekebisho ya sheria yatawasilishwa Bungeni katika kikao cha Bunge lijalo.
“Wizara inapitia sheria ili kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara katika SADC, sheria zote zitapitiwa pia na kufanyiwa marekebisho ili kutengeneza muundo sahihi wa soko,” amesema.
Alisema Tanzania ina historia nzuri ya kuwa nchi yenye amani na pia ushiriki mzuri katika masuala mbalimbali ya kijamii ambayo yakitumika vizuri ni fursa nzuri ya kibiashara.
Waziri huyo pia alisema Mpango Mkakati wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na Biashara nchini (Blueprint) utawasaidia pia wafanyabiashara kufanya biashara zao bila vikwazo.
Chanzo Habarileo