Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Mh. Elibariki Kingu (katikati) akiangalia usafishaji wa dhahabu kwa kutumia mashine duni ya Wachimbaji wa Kata ya Muhintiri alipofanya ziara ya siku moja ya kutembelea machimbo hayo yaliyopo wilayani Ikungi mkoani Singida jana.
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Mh. Elibariki Kingu (katikati) akiangalia mawe yenye dhahabu akiwa na wachimbaji wadogo.
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Mh. Elibariki Kingu (kushoto) akiangalia mchanga wenye dhahabu baada ya kusafishwa.
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Mh. Elibariki Kingu (wa tatu kulia) akipata maelezo kutoka kwa wachimbaji wadogo wakiwa eneo la machimbo.
Wachimbaji wadogo wakiwa eneo la machimbo na Mbunge wao.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WACHIMBAJI wadogo wa madini wa Muhintiri Mining Cooperative Society Ltd wamewaomba wawekezaji ambao watashirikiano nao kuchimba dhahabu katika kata hiyo.
Ombi hilo walilitoa jana wakati wakizungumza na Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu alipofanya ziara ya siku ya kutembelea mgodi wa uchimbaji wa madini uliopo Kata ya Muhintiri katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.
Akizungumza mbele ya Mbunge Kingu, Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa wilaya hiyo, Selemani Dule alisema wanahitaji wawekezaji ambao watashirikiana nao katika kazi.
" Mheshimiwa Mbunge katika mgodi huu tunatumia zana duni za uchimbaji tunaomba ututafutie wawekezaji ambao watasaidia tuwe na uchimbaji wa kisasa" alisema Dule.
Akizungumzia changamoto waliyonayo katika mgodi huo alisema ni uchimbaji holela ambapo walimuomba Kingu awasaidie kupata wataalamu kwa ajili ya kupima ili kuyabaini maeneo yenye dhahabu ili kuwarahisishia uchimbaji.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni mawe yenye dhahabu kuwa ndani ya mto Muhintiri ambao watu wa mazingira waliwashauri waupitishe eneo lingine ili wao waendelee na uchimbaji kwenye eneo hilo.
Mchimbaji mdogo wa eneo hilo Moses Mussa alisema changamoto kubwa waliyonayo ni kuondolewa na mtutu kwenye maeneo wanayoyagundua yana madini na kuchukuliwa na wakubwa ambao hakufafanua ni akina nani.
"Tukigundua madini yalipo wakubwa huwa wanakuja na askari polisi na kutuondoa kwa mtutu jambo ambalo linaturudisha nyuma kiuchumi" alisema Mussa.
Baada ya kusikia changamoto hizo za wachimbaji hao Kingu aliwaahidi kuzifikisha kwa wahusika ili kuzitafutia ufumbuzi.