Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAFUNGWA ZAIDI YA 300 KATIKA MAGEREZA YA MIKOA YA KANDA YA ZIWA WAACHIWA HURU.....WAMO ASKARI 8 WALIODAIWA KUSAFIRISHA SHEHENA YA DHAHABU


Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga, ametangaza kuwaachia huru wafungwa 325 na mahabusi katika magereza ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Kati ya walioachiwa ni pamoja na askari wanane waliodaiwa kupanga njama za kutorosha dhahabu  mkoani Mwanza.

Mganga alitangaza jana uamuzi huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, , akiwa ameambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dk. Agustino Mahiga.

Alisema katika gereza la Butimba amewaachia huru wafungwa na mahabusi 75,  Shinyanga  25, Kahama 43, Mugumu 52, Bunda 24, Bariadi 100 na Tarime 6  huku akiahidi leo atakuwa katika magereza ya Ukerewe na Sengerema.

Alisema  walioachiwa alibainika kubambikiwa kesi, wagonjwa, umri na tuhuma zingine zenye harufu ya rushwa kuanzia kwa raia wenyewe kwa wenyewe, mpelelezi hadi kwa hakimu.

Mganga alisema hatua ya kuwaachia ilifikiwa baada ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na wahusika.

Alisema waliokuwa watumishi wa umma wakiwamo askari polisi watarudishwa kazini isipokuwa kama kutakuwa na kesi nyingine ya msingi.


Askari hao ni Mkuu wa Operesheni mkoa wa Mwanza, Morice Okinda, E 6948 D/CPL Kasala, F 1331 PL Matete, G 6885 D/C Alex na G 5080 D/C Maingu.

Wengine ni G 7244 D/C Timothy, G 1876 D/C Japhet, H 4060 D/C David Kadama ambao walifikishwa mahakamAni hapo kwa mara ya kwanza Januari 11, 2019.

Askari hao pamoja na wafanyabiashara wanne walikuwa wakikabiliwa na makosa matano ya kutakatisha fedha, uhujumu uchumi na kula njama za kupanga uhalifu, makosa waliyodaiwa kuyatenda kati ya Januari 4 na 5, 2019.

Waliokwepa kifungo ni wafanyabiashara Hassan Sadiq ambaye alikuwa mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Emmanuel Mtemi, Kisabo Nkinda na Sajid Hassan.

Kwa upande wake Waziri Dk. Mahiga, alisema katika ziara yake Kanda ya Ziwa ndani ya siku 10, kuwepo urasimu, kubambikiziwa kesi na kulazimishwa kukubali makosa.

 “Kilio kikubwa kwa wananchi ni kucheleweshwa kupata haki kutokana na upelelezi kutokamilika jambo linalosababisha magereza kujazana watu bila sababu, leo imekuwa bahati kwa gereza la Butimba maana tumekutana na Kamishna wa Magareza, DPP na mimi ndio, tumekaa wote na kuamua hivyo.

“Tumekubaliana kutembelea magereza yote nchini na kuwasikiliza wafungwa na mahabusi na kutoa msamaha, magereza yote nchini yameonekana kuzidiwa na yalijengwa miaka ya 1940 huku gereza jipya ni la mwaka 1972 na uwezo wake ni watu 200 lakini kwa sasa yanabeba watu zaidi ya 500,”alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com