WASHITAKIWA WENGINE WATANO RAIA WA KIGENI KUONGEZWA KESI YA KUTEKWA MO DEWJI


Upande wa mashtaka katika kesi ya kutekwa kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’ umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa hati ya kuwakamata washtakiwa watano ili waunganishwe na mshtakiwa wa kwanza, Mousa Twaleb.


Walioongezwa ni raia wa Afrika Kusini, Phila Tshabalala na wenzake wanne raia wa Msumbiji ambao ni, Henrique Simbue, Daniel Berdardo Manchice, Issac Tomu na Zacarious Junior.


Mahakama imetoa hati hiyo leo Jumanne Julai 23,   mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya Wakili wa Serikali, Wankyo Simon kuomba kufanya hivyo.

Washtakiwa hao wanatakiwa kuunganishwa katika shtaka la pili na shtaka la tatu ambapo shtaka la kwanza linamkabili Twaleb ambaye anadaiwa  kujihusisha na genge la uhalifu,  kati ya Mei mosi mwaka 2018 na Oktoba mwaka huo Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Johannesburg Afrika Kusini.

Inadaiwa shtaka la pili la kujihusisha na genge la uhalifu linamuhusu washtakiwa wote wanaosakwa ili wafikishwe mahakamani.

Shtaka la tatu washtakiwa wote wanadaiwa kuteka nyara, inadaiwa Oktoba 11 mwaka 2018 katika Hoteli ya Colleseum wilayani Kinondoni, akiwa pamoja na wenzake walimteka mfanyabiashara, Mohammed Dewji kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri kinyume cha sheria.

Mshtakiwa Twaleb katika shtaka la nne wanadaiwa kutakatisha fedha Sh milioni nane, inadaiwa Julai 10 mwaka jana maeneo ya Mbezi Beach alijipatia kiasi hicho cha fedha huku akijua fedha hizo ni mazalia ya genge la uhalifu. Kesi itatajwa Agosti 6 mwaka huu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post