WATATU KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA KUJIFANYA MAOFISA WA TAKUKURU


Mkuu wa kitengo cha mauzo Hoteli ya Ramada,  William Mgatta (36) na wenzake wawili wamefikishwa katika   Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kujifanya maofisa wa Takukuru na kushawishi rushwa ya Sh300 milioni.

Mgatta na wenzake Mohammed Abdallah (25) na Daniel Ileme (35) wanakabiliwa na kesi ya jinai kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo  jana Jumanne Julai 16, 2019 na  kusomewa mashtaka  yao mbele ya Hakimu Mkazi, Agustina Mmbando.
 

Hati ya mashtaka ilisomwa na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Aneth Mavika  ambapo alidai kati ya Mei Mosi na  Juni 10, mwaka huu, katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Arusha, mshitakiwa Abdallah na Ileme wakiwa wafanyabiashara na mshitakiwa Mgatta akiwa Mkuu wa Kitengo cha mauzo cha Ramada hoteli walishawishi rushwa ya Sh milioni 300.

Alidai kuwa, alishawishi rushwa hiyo kutoka kwa Francis Matunda kama kishawishi ili wasimchukulie hatua za kisheria kwa kukataa kuwalipa wafanyakazi wake kiasi cha Sh bilioni moja wanayomdai.

Imeendelea kudaiwa kuwa katika tarehe tofauti katika eneo lisilotambulika jijini Dar es Salaam na Arusha washitakiwa Abdallah, Ileme na Mgatta walikula njama ya kutenda kosa la kujifanya ni watumishi wa umma.

Wakili Mavika aliendelea kudai kuwa, katika shtaka la tatu, imedaiwa, Juni 10, mwaka huu katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam na Arusha washtakiwa kwa pamoja  walijifanya ni watumishi wa Takukuru kitu ambacho walijua kuwa si kweli.

Hata hivyo, upande wa mashtaka umedai kuwa, upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na hawana pingamizi la dhamana endapo washitakiwa watatimiza masharti.

Akiwasomea masharti ya dhamana, Hakimu Mmbando alimtaka kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika wenye barua halali na vitambulisho ambao pia wametakiwa kuwalisilisha mahakamani hapo fedha taslimu Sh milioni 50 au hati ya mali isiyohamishika  yenye thamani ya fedha hiyo na kusaini bodi ya Sh milioni 50.

Washitakiwa walishindwa kutimiza masharti hayo na wamerudishwa rumande. kesi imeahirishwa hadi Julai 30, mwaka huu .


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post