Watoto, akiwamo mmoja wa miaka 10, wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, walivyoshuhudia baba yao wa kambo, Godfrey Nkwambi, akimnyonga mama yao Bahati Hussein.
Watoto hao, huku wengine wakibubujikwa machozi, walitoa ushahidi huo jana katika kesi ya mauaji inayomkabili Nkwambi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Msajili Pamela Mazengo.
Mtoto Hassan Hussein (10) alidai kwamba alimwona baba yake wa kambo, Godfrey Nkwambi, akimnyonga mama yake na kumwamuru asipige kelele.
Hassan ambaye alilala chumbani kwa mama yake (wakati huo akiwa na miaka mitano), alidai kuwa siku ya tukio alimwona baba yake wa kambo ni mshtakiwa katika kesi hiyo, alitoa madai hayo wakati akitoa ushahidi dhidi ya mauaji hayo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Erick Shija, shahidi huyo alidai siku ya tukio akiwa amelala chumbani kwa mama yake chini kwenye godoro pamoja na mdogo wake aliyemtaja kwa jina la Ibrahim, kwa kawaida mama yake na baba yake wa kambo walikuwa wakilala kitandani.
Siku ya tukio, alidai kuwa usiku alishtuka na alimuona mshtakiwa (baba wa kambo) akimnyonga mama yake na alimwambia asipige kelele na mama yake alikuwa akitikisa miguu huku akitoa sauti kwa mbali.
"Nililala lakini niliposhtuka nilimwona mshtakiwa akifanya hivi halafu hivi (alionyesha mahakama mikono ya mshtakiwa ilivyokuwa imeshika kichwa na kidevu na kukizungusha). Mama alikuwa akipiga miguu kitandani na kutoa kelele kwa mbali, God aliniambia nisipige kelele, mimi nikanyamaza, nikamwona akitoka nje sikujua kilichoendelea kwani niliendelea kulala hadi asubuhi," alidai Hussein.
Alidai kuwa asubuhi alimwacha mama yake akiwa bado amelala, yeye akatoka nje kupiga mswaki na baadaye alikwenda kucheza.
"Siku hiyo sikumwona Godfey na sikujua alikokwenda lakini baadaye nilisikia watu wakilia nyumbani kwetu, ndugu zangu wakaniambia mama yetu mzazi amefariki (dunia)," alidai shahidi huyo na kusababisha ndugu wa marehemu waliofika mahakamani kusikiliza kesi hiyo kuanza kutoa machozi.
Shahidi mwingine ni mtoto wa marehemu, Khadija Abibu (15), aliieleza mahakama kuwa mama yake alifariki dunia Juni 21, 2014 na kwamba Juni 20 alipotoka kucheza alikuta baba yake (mshtakiwa), mama yake na watu wengine wakiwa wamekaa katika mkeka nyumbani kwao Ulongoni.
Alidai kuwa dada yake anayeitwa Hadija Shabani, alimwambia kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya baba na mama yake ambao ulisuluhishwa na kwisha na baadaye alimshuhudia mshtakiwa akimpa fedha mama yake akanunue mboga kwa ajili ya chakula cha usiku.
Alidai kuwa majira ya saa 5:00 usiku, alikwenda kuwalaza wadogo zake, Hassan na Rahim, chumbani kwa mama yao na kisha akaenda kulala chumbani kwake pamoja na mtoto wa mama yake mdogo.
"Usiku nilishtuka nikasikia mama na Godfrey wanagombana. Mtoto wa mama mdogo alikuwa anaogopa, nikamwambia yataisha sisi tulale, tukabaki macho kitandani. Mtoto wa mama mdogo akabanwa na haja ndogo, hivyo tukatoka nje kujisaidia," alidai Khadija.
Alidai kuwa walipotoka nje walimwona Godfrey akiwa amekaa katika kochi sebuleni akiwa amevaa kipensi, shati begani huku akitokwa na jasho na kuwahoji wanakokwenda.
"Sisi tulimjibu tunaenda kujisaidia, akasema haya. Tuliporudi tukasikia Godfrey akifungua mlango wa sebuleni na kutoka nje, sisi tulijificha nyuma ya mlango wa sebuleni, tulimsikia Godfrey akimgongea mpangaji wa chumba cha nje na kumuuliza kama alisikia kelele, yule mpangaji akamwambia hakusikia kelele," alidai shahidi.
Shahidi huyo alidai, baadaye walienda kulala, asubuhi aliamshwa na mama mwenye nyumba ambaye alimtaka achukuwe beseni la vyombo apeleke chumbani kwa mama yake.
Huku akitokwa na machozi, shahidi huyo alidai aligonga mlango lakini mama yake hakuitikia na alipoingia ndani alimkuta mama yake amelala akiwa amefunikwa shuka jeupe na kanga kichwani, alimtikisa hakuamka na kutoka nje huku akipiga kelele.
"Nilikuta mama kalala, niliendelea kumwamsha bila mafanikio, nikamfunua alikuwa hajavaa nguo, nikamshika kifua kuona kama roho yake inadunda, ilikuwa haidundi, nikatoka nje nikipiga kelele. Mama mwenye nyumba aliniuliza nikamwambia mama yangu hahemi amefunikwa nguo, majirani walikuja na kumwangalia, wakasema atakuwa amezimia, wakamvalisha nguo na kumpeleka hospitalini," alidai.
Khadija alidai kuwa watu waliorudi kutoka hospitalini walimwambia kuwa mama yao amekufa na alinyongwa. Alidai kuwa mama yake alinyongwa na Godfrey kwa sababu alishawahi kumtamkia kuwa atamuua yeye na familia yake kwa kuwa hataki kuiona.
"Mama pia alishawahi kuniambia kwamba, 'mwanangu nikifa Godfrey ndiye kaniua," alidai.
Naye shahidi Khadija Shabani, ambaye alikuwa akimwita marehemu shangazi, aliieleza mahakama kwamba wawili hao walikuwa na ugomvi na kwamba Godfrey alikuwa akimtuhumu Bahati kuwa na uhusiano wa kimapenzi na jirani yao.
Social Plugin