Watu 12 wakazi wa sehemu tofauti jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kukwepa kodi na kusababisha hasara ya zaidi ya sh. Milioni 100.7/-
Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa serikali, Janet Magoha amewataja washtakiwa hao kuwa ni, Rose Kerandi, Ally Abdul, Geoffrey Kayanza, Anwar Rubeya, Khalid Kigoma, Joseph Marcelo, Samir Hussein, Matiku Mgaya Iddi Bogaboga, Edward Maguri, Alex Sanga, Said suleman, Lali Mohamed na Hamidu Abu.
Imedaiwa mbele ya Hakimu Mkazi Salum Ally kuwa, Siku na mahali pasipo julikana, washtakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa la kukwepa kodi.
Katika shtaka la pili imedaiwa February 21, 2019 ndani ya jiji la Dar es Salaam, washtakiwa walishindwa kulipa kodi ya sh. 100,739,873 ya mzigo wa ambao walikuwa wakiuingiza nchini.
Pia washtakiwa hao wanadaiwa, Siku na mahali hapo waliisababishia TRA hasara ya kiasi hicho cha fedha kwa nia ovu ya kutokulipa kodi ya bidhaa ya kontena la futi 40 lilolokuwa limebeba mikoba.
Hata hivyo wakato wakisomewa mashtaka hayo, washtakiwa Anwary Rubeya, Joseph Marcelo, Matiku Mgaya na Idd Bogobogo hawakuwepo mahakamani hapo na mahakama imetoa hati ya wa washtakiwa hao kukamatwa ili waweze kufika mahakamani hapo kujibu mashtaka yao.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu Uchumi na imeahirishwa hadi Agosti 6, mwaka huu.
Kwa mujibu wa upande wa utetezi, upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika, washtakiwa wote wamerudishwa rumande.
Social Plugin