NA.MWANDISHI WETU - OWM
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchi Mhe. Angellah Kairuki ameutaka uongozi wa Kiwanda cha kutengeneza marumaru cha GoodWill Tanzania ceramic ltd kuzingatia ustawi wa wafanyakazi wake kwa kuzingatia kanuni na sheria mbalimbali za ajira nchini ili kuendelea kuwa mazingira mazuri ya wafanyakazi wake.
Ametoa kauli hiyo alipofanya ziara yake mwishoni mwa wiki katika kiwanda hicho kilichopo katika Kijiji cha Mkiu kata ya Nyamato Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani.
Waziri Kairuki alieleza kuwa, upo umuhimu wa kujali wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi kwa kuzingatia usalama na afya mahala pa kazi ili kuondokana na mazingira mabaya yanayoweza kukwamisha uzalishaji unaotarajiwa.
“Ikiwa kiwanda kimeweza kutoa ajira zipatazo 3000 ni idadi kubwa hivyo lazima myatazame mahitaji yao na kuendelea kuzingatia sheria na haki za wafanyakazi wawapo kazini,”Alisema Waziri Kairuki.
Aliongeze kuwa miongoni mwa maeneo muhimu kwa wafanyakazi wenu ni kuhakikisha mnawapa mafunzo kazini ili kuongeza ujuzi katika fani mbalimbali zinazoendana na uzalishaji kiwandani hapo.
Aidha aliwataka kuendelea kuwapa motisha na kuwa na njia za ubunifu katika kuhakikisha kila mfanyakazi anakuwa mwenye ustawi na kufurahia mafanikio ya uwepo wa kiwanda hicho.
“Ni lazima kujali masuala ya usalama wa afya zao wawapo kazini, kujali stahiki zao, kuwapa kazi zenye staha kwa kulingana na kanuni na sheria za kazi zilizopo,”alisisitiza Waziri Kairuki
Naye Meneja Mwajiri wa kiwanda hicho Bw. Figa Msaphiry alimpongeza Waziri kwa Ziara yake kiwandani hapo na kuahidi kuendelea kuyatekeleza maagizo hayo ikiwemo la kuhakikisha wanaendelea kujali masuala ya Afya na Usalama Mahala Pa Kazi kwa kuzingatia mchango unaotolewa na wafanyakazi hao katika kiwanda hapo.
Alifafanua kuwa, kiwanda kimefanikiwa kutengeneza ajira za moja kwa moja kwa watanzania 936 kati ya hao wanaume 887 na wanawake 49, lakini pia kiwanda kimetengeneza ajira zisizo rasmi Zaidi ya 1,500 na kwa siku wanapokea vibarua ambao wapatao 40 hadi 50 na hii kupeleekea kuongeza fursa za ajira nchini.
Aliongeze kuwa wafanyakazi wamechangia matokeo chanya katika uzalishaji ambapo kiwanda kinazalisha marumaru mita za eneo 40,000 mpaka 50,000 kwa siku kuwa ambapo soko la ndani ni kwa asilimia 30 hadi 40 na soko la nje ni kwa asilimia 60 hadi 70.
“Kiwanda chetu kimeweza kupanua soko la marumaru kwa kuuza katika nchi za nje, kwani kwasasa kiwanda kinauza marumaru katika nchi za Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Congo kwa kuzingatia ubora wa bidhaa zetu,”alieleza Figa .
kiwanda cha Good Will Company Limited kilijengwa mwezi Machi, 2016 na kuwekwa jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hiki na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kasimu Majaliwa, na kuanza uzalishaji wake mnamo Mwezi Aprili Mwaka 2017.Kiwanda kinazalisha marumaru za sakafuni (floor tiles) na marumaru za ukutani (wall tiles) kwa saizi zote na “scating”, Katika uzalishaji wa marumaru kiwanda kinatumia malighafi tofauti tofauti ambapo 95% ni malighafi toka hapahapa Tanzania na 5% kutoka China ambazo ni kemikali.Malighafi zinazotoka Tanzania ni felidisper ambayo inatoka Tanga – Handeni, Morogoro na Dodoma, nyingine ni Soap stone kutoka Dodoma na Morogoro, Magnesite kutoka Same Moshi, Udongo wa mfinyanzi (clay soil) na udongo mwekundu (red soil) kutoka Mkuranga – Pwani, Limestone kutoka Mavuji – Kilwa na Kaolin kutoka Kisarawe Pwani. Mradi huu wa ujenzi wa kiwanda umegharimu jumla ya fedha za kigeni dola milioni 50.
Social Plugin