Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka, Biswalo Mganga, wameshangazwa wafungwa watu wazima kuchanganywa na watoto chini ya miaka 18 magerezani mikoa ya Simiyu na Mara.
Mbali na hilo, viongozi hao wameshangazwa pia kukuta idadi kubwa ya watu waliopo magereza ya mikoa hiyo, robo tatu wakiwa ni mahabusu huku wengine wakiwa ni wafungwa kamili baada ya kuhukumiwa.
Tukio hilo limetokea jana mara baada ya viongozi hao kuhitimisha ziara ya kikazi ya kuangalia mazingira ya utoaji haki na haki jinai mikoa ya Simiyu na Mara.
Katika ziara hiyo iliyoaanza Julai 9 hadi jana, viongozi hao walitembelea magereza ya Tarime, Mugumu-Serengeti, Bunda na Bariadi na kuongea na wafungwa, watumishi wa mahakama, polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Tulikutana na watoto wote tuliowakuta kwenye magereza hayo na kusikiliza kesi zao, ambapo DPP alitoa uamuzi wa kuwafutia kesi baadhi yao,” alisema Balozi Mahiga.
DPP Mganga alisema utaratibu wa kuwachanganya watoto wadogo na watu wazima magereza unakinzana na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, ambayo inataka wapelekwe gereza la watoto.
“Kutokana na mazingira ya nchi pamoja na kesi za watoto hao, tumewaelekeza watu wa magereza kuwatengea maeneo yao maalumu, kuwepo kwa gereza lao, pamoja na askari wa kuwahudumia ambao wamepewa mafunzo ya kuwatunza.
“Vile vile tunaomba jamii ibadilike na kuwalea watoto wao katika mienendo mizuri ili wasijiingize katika uhalifu, kwani huko pia tumewakuta watoto wenye kesi za mauaji, huku wengine wakiwa na kesi za kawaida ambazo tumezifuta na wameachiwa huru,” alisema.
DPP Mganga alisema kuna baadhi kulingana na mazingira ya kesi zao hawakuweza kuwafutia ila wameelekeza wawekwe katika mazingira maalumu kama sheria inavyotaka.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao pia walibainisha kuwa baadhi ya wafungwa waliwataja watumishi wa magereza kujihusisha na vitendo vya rushwa, na Dk. Mahiga aliagiza mamlaka za uchunguzi kufanyia kazi tuhuma hizo kisha kuwachukulia hatua kali wahusika.