Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MBARAWA AANZA KWA KASI UTEKELEZAJI WA AGIZO LA RAIS


Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amewahakikishia wananchi wa Kyaka, Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera kupata huduma ya majisafi na salama kutoka Mto Kagera ifikapo Desemba, 2019.

Kauli hiyo aliitoa Julai 12, 2019 wakati wa ziara yake Wilayani humo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa Julai 11, 2019.

Akiwa njiani akitokea Wilayani Karagwe kuelekea Wilayani Chato, Rais Magufuli alisimama katika Mji Mdogo wa Kyaka kusalimiana na wananchi na walimueleza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama.

Rais Dkt. Magufuli alimuagiza Waziri Mbarawa kwa njia ya simu mbele ya wananchi hao kufika eneo hilo siku iliyofuata kuzungumza nao na kuhakikisha kero hiyo inatatuliwa na ikifika kipindi cha Sikukuu ya Krismasi mwaka huu wananchi hao wawe wamepata huduma ya majisafi na salama.

Katika utekelezaji wa agizo hilo, Waziri Mbarawa akiwa ameongozana na Watendaji na Wataalam kutoka Mamlaka za Maji Mwanza (MWAUWASA) na Bukoba (BUWASA) alisisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuwaondolea wananchi wake kero ya maji na aliwahakikishia wananchi wa Kyaka kwamba kero ya maji inakwenda kuwa historia.

Profesa Mbarawa alisema Mkandarasi mahiri atapewa jukumu hilo la kujenga mradi wa maji na aliwasihi wananchi hao wa Kyaka kutakapojengwa chanzo cha maji kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi atakayetekeleza mradi ili ukamilike kwa wakati na kwa kiwango.

"Tumesema sasa imetosha wananchi kuhangaika, tunawahakikishia wananchi wote wa Kyaka kuwa  mtapata majisafi na salama kutoka Mto Kagera, tunajenga mradi mkubwa wa maji ambao pia ni endelevu," alisema Waziri Mbarawa.

Waziri Mbarawa aliamuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga kushirikiana na Mkurugenzi wa Maji Bukoba, Allen Marwa na wataalam wengine kutoka Wizara ya Maji kusimamia na kuratibu haraka shughuli za awali za ujenzi wa mradi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa MWAUWASA, Mhandisi Sanga alielezea walivyojipanga kwenye maandalizi ya awali ya ujenzi wa mradi.

Mhandisi Sanga alibainisha kwamba shughuli za awali za utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na kumpata Mkandarasi wa ujenzi zitakamilika ndani ya muda mfupi ili kazi za ujenzi ziweze kukamilika katika muda ulioelekezwa na Rais Dkt. Magufuli.

"Ili kukamilisha ujenzi wa mradi katika kipindi kilichoagizwa na Mhe. Rais inatakiwa taratibu za awali zifanyike kwa muda mfupi kadri iwezekanavyo ikiwa ni pamoja na kumpata mkandarasi atakaye jenga mradi," aliongeza Mhandisi Sanga.

Kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha wananchi wa maeneo ya Kyaka, Bunazi na maeneo mengine ya Mutukula, Kakunyu na Bubale.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com