Na. OWM, DODOMA.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, amelitaka Baraza la Vyama vya siasa nchini kuendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu juu ya masuala yenye maslahi kwa Taifa kuhusiana na vyama vya siasa pamoja na hali ya kisiasa nchini ili kuimarisha ustawi wa siasa na vyama vya siasa nchini.
Mhe. Waziri Mhagama ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha siku mbili cha Baraza hilo kilichoanza jana na kinafungwa leo, tarehe 24, Julai 2019, mjini Dodoma katika ukumbi wa Pius Msekwa, ambapo Mhe. Mhagama amesisitiza vyama hivyo kuendelea kushirikiana na kudumisha upendo na umoja wa kitaifa katika kutekeleza majukumu yao ya kisiasa ili kuweza kuijenga Tanzania yenye umoja.
“Endeleeni kutumia fursa za vikao vya Baraza kutatua matatizo yenu na niwashauri muunde kamati za Baraza na kutumia kamati hizo katika kutatua matatizo yenu, lakini pia tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu tulizonazo hapa nchini ili vyama viweze kuisaidia nchi na watanzania kuyafikia malengo yao kwa kuwajenga watanzania kuwa wamoja badala ya kuwagawanya” amesema Mhagama
Mhe. Waziri Mhagama amefafanua kuwa katika vikao vyao na serikali Baraza hilo walikuwa na matakwa yao ambayo walitaka serikali iyatekeleze kupitia ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini ambapo tayari serikali imeyatekeleza ikiwemo kuanzisha ofisi ya Naibu msajili wa vyama vya siasa Zanzibar.
“Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, katika bajeti yake, ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa, tayari imetenga bajeti ya kuiendesha Ofisi ya Naibu Msajili wa vyama vya siasa Zanzibar, lakini pia sisi serikalini tumeshakubaliana kuwashirikisha viongozi wa Baraza la vyama vya siasa katika matukio ya shughuli za maendeleo ya serikali ili viongozi nyie muweze kuelewa vyema mabadiliko ya utekelezaji yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano” Amesisitiza Mhe. Mhagama.
Aidha, Mhe. Mhagama ameeleza kuwa Wajumbe wa Baraza hilo watakuwa wakijengewa uwezo katika masuala ya siasa ili kuweza kuendelea kujenga msingi imara na ustawi wa demokrasia nchini.
Awali, akiongea katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza hilo, John Shibuda, ameeleza kuwa wanashukuru kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiupata kutoka serikalini kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa ambapo ameomba kuendelea kushirikishwa ipasavyo ili waweze kuelewa vyema utekelezaji wa shughuli za maendeleo za serikali ya awam ya tano.
“Baraza tunamshukuru sana Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Mhagama kwa ushirikianao ambao amekuwa akitupatia Baraza kimsingi hivi leo tunajivunia miaka miwili ya utendaji wa Baraza letu lakini msingi wa mafanikio hayo ni Waziri huyu amekuwa ufungua ambao atufungulia milango kila jambo tunalotaka kulitekeleza kwa wakati ” amesema Shibuda.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini, Mhe. Jaji Francis Mutungi, Naibu Msajili wa Vyama vya siasa, Mhe. Mohammed Ally Ahmed, pamoja na wajumbe wa Baraza hilo ambao ni vyama vyenye usajili wa kudumu. Baraza la Vyama vya Siasa limeanzishwa chini ya kifungu cha 21B cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 ikiwa ni jukwaa la viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa kukutana mara kwa mara kujadiliana masuala yanayohusu demokrasia ya vyama vingi na siasa hapa nchini kwetu. Baraza hilo limeundwa ndani ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambapo, Wajumbe wa Baraza hilo hujumuisha viongozi wa kitaifa wawili wa kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa ndio yenye jukumu la kisheria ya kuratibu shughuli za Baraza la Vyama vya Siasa.
Majukumu ya Baraza hilo ni pamoja na kumshauri Msajili wa vyama vya siasa juu ya masuala yenye maslahi kwa Taifa kuhusiana na vyama vya siasa au kuhusiana na hali ya kisiasa nchini Siasa na sheria zingine zinazohusu masuala.