Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AAGIZA ENEO LA MNARA WA ZINJATHROPOUS LIBORESHWE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii isimamie uboreshaji wa eneo la mnara wa Zinjathropus ili paweze kuvutia zaidi.


Ametoa agizo hilo jana mchana (Jumatatu, Julai 22, 2019) wakati akizungumza na wananchi na viongozi waliohudhuria maadhimisho ya miaka 60 ya kumbukizi ya ugunduzi wa fuvu la Zinjathropus Bosei, eneo la bonde la Olduvai, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha.

Maadhimisho hayo yamefanyika ndani ya hifadhi ya Ngorongoro sambamba na uzinduzi wa makumbusho ya Dkt. Mary Leakey. Mnara wa Zinjathropus na Homo habilis umejengwa kwenye hifadhi ya Ngorongoro karibu na njia panda ya kuelekea bonde la Olduvai.

“Kwenye mnara wa Zinjathropus na Homo habilis pasiachwe kama palivyo. Pajengwe seng’eng’e kuzunguka eneo lile lakini pia paweke kibanda cha mlinzi ambaye pia atakuwa anatoa taarifa kwa wageni wanaopita hapo.”

“Mtafute vijana kadhaa ambao ni wenyeji wa eneo hili, wafundishwe historia kamili kisha wapewe ajira hizo. Kibanda kikijengwa kwa juu kiwe na vioo ili anayelinda aweze kuona pande zote na pia muweze kumkinga na vumbi na upepo mkali wa eneo lile.”

Waziri Mkuu pia alitembelea korongo la Frida Leakey, (mahali ambapo zinjathropous aligunduliwa) na kupata maelezo juu ya kugunduliwa kwa fuvu la mtu wa kale duniani yapata miaka milioni mbili iliyopita.

Akigusia kuhusu uhifadhi wa eneo hilo, Waziri Mkuu alisema nako pia pajengwe kibanda cha mlinzi mwenye uwezo wa kutoa taarifa kwa watalii na akasisitiza pia ajira hizo ziwahusu wenyeji wa eneo hilo.

“Kwenye korongo la Frida, pawekwe bango lenye maelezo ya Kiswahili, nako pia wapatikane vijana sita au nane, waeleweshwe hiyo historia, wakifuzu, Wizara iwawezeshe, wapangiane zamu ya kushinda hapo. Pia pajengwe kibanda cha wageni kupumzikia wakifika eneo hilo.

Kuhusu makumbusho ya Dkt. Leakey, Waziri Mkuu alisema makumbusho hayo ni lulu kwa Taifa. “Ninawapongeza viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Ngorongoro kwa kuendeleza na kutunza makumbusho haya.”

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangallah alisema kwa sasa dunia inatambua kuwa chimbuko la binadamu ni Afrika. “Hata kama tunatofautiana sura na rangi, watu wote duniani wana asili ya Afrika. “Kwetu sisi Tanzania, tunaadhimisha uvumbuzi huu kwa sababu fuvu la Zinjanthropus ni alama na nembo ya Tanzania na dunia.”

Alisema maadhimisho hayo yataendelea kwa kufanya maonesho ya fuvu la Zinjanthropus boisei na malikale zingine katika mikoa sita ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Iringa, Mtwara na Dodoma.

Alisema wizara yake imebaini fursa zilizopo kwenye sekta ya urithi wa utamaduni yaani malikale au utamaduni tuli (static cultural heritage) na utamaduni hai (dynamic culture) ili  kuvutia watilii na hivyo kuongeza idadi yao na kuwafanya waongeze muda wa kukaa nchini (length of stay) na hatimaye kuongeza pato la Taifa litokanalo na utalii.

“Wizara yangu imeanza kuiboresha na kuendeleza sekta ya malikale na urithi wa utamaduni ili izalishe mazao ya utalii na kuvutia watalii kwa kuhamisha vituo vya Idara ya Mambo ya Kale na kuvipeleka TANAPA, TAWA, NCAA, TFS na Makumbusho ya Taifa ili viendelezwe na kuwa vivutio vya utalii.

“Pia tumehamishia Makumbusho ya Taifa kazi zote za uhifadhi wa urithi wa utamaduni tuli au malikale na kuanzisha tamasha la urithi wa utamaduni wa Mtanzania (Urithi Festival: Celebrating Our Heritage).  Tamasha hili litasherehekewa Septemba, kila mwaka.

Naye Balozi wa Marekani hapa nchini, Dk. Inmi Patterson ameipongeza Serikali kwa kukuza na kuendeleza utalii wa kitamaduni.

Pia alisifu utajiri wa rasilmali misitu na wa nyama ambao Tanzania imejaliwa kuwa nao. “Uamuzi wa Rais Magufuli wa kuanzisha hifadhi ya Burigi, unazidi kunogesha sifa ya Tanzania katika suala la hifadhi za maliasili na utalii na katika kukuza urithi na utajiri wa nchi,” alisema kwa Kiswahili fasaha.

Alisema maadhimisho hayo ni siku muhimu kwake kwani yamewakutanisha watu wa kaliba tofauti wakiwemo wanasiasa, wanasayansi, maprofesa kutoka Uingereza, Marekani na Ujerumani, wanafunzi kutoka shule za Tanzania na wenyeji wa Ngorongoro.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com