Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo - Dar es salaam
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 5 Julai 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya TOPIC ya Mjini Cairo nchini Misri Mhandisi Raouf Bakry katika kikao kazi kilichofanyika Ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam.
Katika mkutano huo Mhandisi Raouf amemueleza Mhe Hasunga kuwa lengo la ziara yake ni kuangalia uwezekano wa kutumia fursa inayopatikana na kutolewa na Benki ya EXIM inayotoa mikopo nafuu ili kufanya biashara kati ya nchi za Afrika.
Amesema kuwa akipatiwa mkopo huo ataongeza uwezekano wa kusambaza mbolea na viuatilifu ili kuongeza tija na kasi ya uzalishaji wa mazao mbalimbali ya wakulima.
Kwa uoande wake Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amemueleza Mhandisi Raouf kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kutekeleza kwa vitendo hivyo ina wakaribisha wawekezaji katika uwekezaji mbalimbali ikiwemo sekta ya viwanda vya kusindika mazao.
Alisema kuwa Mhe Magufuli amejipambanua katika kuimarisha uwezekano wa wawekezaji kuwa na uwekezaji uliotukuka ili kuwanufaisha watanzania sambamba na manufaa kwao wenyewe.
Katika mkutano huo baina ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya TOPIC ya Mjini Cairo nchini Misri Mhandisi Raouf Bakry ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya mbolea ya Taifa (TFC) Ndg Salum Mkumba.
Social Plugin