Ajali iliyotokana na utaratibu wa matengenezo ya kawaida imetajwa kuwa chanzo cha watumiaji wa mitandao ya WhatsApp, Facebook na Istagram juzi kushindwa kutuma wala kupokea picha, video na mafaili mengine.
Jana kampuni inayomiliki mitandao hiyo ya Facebook ililazimika kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo ikisema sasa tatizo hilo limetatuliwa na mitandao hiyo imerudi kwa asilimia 100.
Juzi baada ya tatizo hilo kutokea kulikuwa na maneno na hisia nyingi, kwamba huenda mitandao hiyo imedukuliwa.
Shirika la Kijasusi la Marekani la CIA lilipata wakati mgumu na hata kuamua kujibu shutuma zilizoelekezwa kwake kupitia mtandao wa Twitter.
“Ndio, nasi pia tumeathirika na mtandao wa Instagram kuwa chini, hapana sisi hatujasababisha, La hatuwezi kurekebisha shida yako, je umejaribu kuzima na kuwasha tena? ” CIA waliandika kujibu maswali ya watu waliokuwa wakiwashutumu kupitia Twitter.
Msemaji wa Facebook, ambaye pia alizungumza kwa niaba ya Instagram na WhatsApp, alifafanua kuwa;
“Matengenezo ya kawaida ya kila siku kwa bahati mbaya yalisababisha hitilafu kwa watumiaji kushindwa kupakua au kutuma picha na video”.
Kwa mujibu wa DownDetector, ambao ni wafuatiliaji wa huduma za mitandao, maelfu ya watumiaji wa WhatsApp, Instagram na Facebook waliripoti shida hiyo juzi baada ya kutokea hitilafu.
Facebook pamoja na kusema wamerejea kwa asilimia 100 walikiri shida hiyo kuathiri watu katika maeneo mengi duniani.
Jumatano DownDetector waliripoti kuwa shida hiyo ilianza karibu saa 6: 00 nchana na iliathiri Facebook pamoja na huduma za Instagram na WhatsApp.
“Tumekwishatatua shida iliyotokea na tumerudi kwa asilimia 100 kwa kila mtu,” iliandika kampuni hiyo katika ukurasa wake wa Twitter saa 6:00 jana usiku, na kuongeza kuwa wanaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza.
Juzi hiyo hiyo, Twitter nao walisema walikuwa wanapitia hali kama ile ile iliyowakuta watumiaji wa WhatsApp, Istagram na Facebook.
“ Tuna shida na DM. tunafanyia kazi na tutawajulisha mara moja tukiishatatua. Tunaomba radhi kw usumbufu wowote” ulisomeka ujumbe wa Twitter siku hiyo hiyo ya Jumatano.
Kwa mujibu wa DownDetector, maelefu ya watumiaji duniani kote waliripoti shida hiyo huku Ulaya na Amerika ya Kaskazini ikiwa ndiyo iliyoathirika zaidi.
Si tu kwa mtumiaji mmoja mmoja, biashara na kampuni pia ziliathirika na tatizo hilo.
Mapema mwaka huu tatizo kama hilo lililodumu kwa saa 24 liliikumba Facebook huku sababu ikitajwa kuwa ni mabadiliko ya kwenye ‘server’.
Tatizo hilo ambalo lilitokea Machi 13 , mwaka huu linaaminika kuwa baya zaidi kuwahi kuikumba kampuni hiyo kubwa ya intaneti inayowafikia watu wanaokadiriwa bilioni 2.7.
Via >>Mtanzania
Social Plugin