Na Munir Shemweta
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameanza operesheni maalum ya kuzibana Taasisi ambazo ni wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi katika jiji la Dara es Salaam kwa kutembelea ofisi moja hadi nyingine ili zilipe madeni yao katika muda uliopangwa ambapo katika ziara hiyo taasisi sita kati ya saba alizotembelea zimeahidi kulipa zaidi ya bilioni 4.5 kufikia Desemba 2019.
Dkt Mabula alizitembelea taasisi hizo juzi ikiwa ni mkakati wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha wadaiwa wote sugu wa kodi ya pango la ardhi wanalipa madeni yao kabla ya hatua za kuwafikisha kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya wale watakaokaidi kulipa ambapo adhabu yake ni kulipa ama kupigwa mnada kwa mali za taasisi husika kufidia deni la kodi ya pango la ardhi.
Taasisi alizotembelea Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi juzi ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linalodaiwa bilioni 3, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) bilioni 1.4, EPZA milioni 200, Shirika la Reli Tanzania (TRC) bilioni 2.5, Shirika la Masoko Kariakoo milioni 249 pamoja na Chuo cha Taifa cha Utalii milioni 26.8.
Akiwa katika Shirika la Masoko Kariakoo, Dkt Mabula alishangazwa na Shirika hilo kudaiwa zaidi ya milioni mia mbili huku likiomba kulipa deni lake katika kipindi cha miaka miwili jambo alilolieleza kuwa ni kinyume na taratibu za ulipajia madeni ya kodi ya pango la ardhi ambazo humtaka mdaiwa kulipa nusu ya deni.
Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo Bw. Hetson Kipsi katika barua yake, Shirika lake liliahidi kulipa kwa awamu deni hilo katika kipindi cha miaka miwili kwa kutoa milioni saba kila mwezi jambo lililokataliwa na Dkt Mabula ambapo alieleza kuwa Shirika hilo linapaswa kulipa nusu ya deni kwanza ndipo liingia makubaliano ya kulipa kiasi kilichobaki kwa awamu. Hata hivyo Shirika la Masoko Kariakoo lilikubali kutoa milioni mia moja kufikia 29 Julai 2019 na kukamilisha kiasi kilichobaki desemba 2019.
Kwa upande wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mkurugenzi Mtendaji wake Masanja Kadogosa alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Mkazi Dkt Mabula kuwa Shirika lake halipingi kulipa deni inalodaiwa bali inachofanya ni kuhakiki upya deni hilo kwa kuwa kumekuwa na uhamisho wa umiliki wa mali za TRC kwenda TBA tangu mwaka 1999 sambamba na baadhi ya nyumba za Shirika kuuzwa kwa wananchi huku baadhi ya mali za TRC zikiwa hazina hati.
Kadogosa alisema, kiasi cha shilingi bilioni 2.4 wanachodaiwa ni kikubwa na hakilingani na uhalisia wa deni la TRC na kubainisha kuwa uhakiki utakapokamilika ana imani deni hilo litapungua kwa kiasi kikubwa. Dkt Mabula alimueleza kuwa, Shirika lake linapaswa kulipa robo ya tatu ya deni hilo wakati uhakiki ukiendelea na iwapo itaonekana deni limepungua basi kiasi cha fedha kilichozidi kitarudishwa. Hata hivyo, Mkurugenzi huyo Mtendaji wa TRC alikubali kulipa kiasi cha milioni 400 kwa awamu hadi kufikia oktoba 2019 wakati zoezi la uhakiki wa deni hilo unaohusisha Wataalamu wa Shirika hilo na Wizara ukiendelea.
Chuo cha Taifa cha Utalii kupitia kwa Kaimu Mkuu wa Chuo Boniface Mwaipaja kilikiri kudaiwa kiasi cha milioni 26.8 na kuahidi kulipa kwa awamu deni hilo ambapo Mkuu huyo wa Chuo aliahidi kulipa kiasi cha milioni saba kwanza na baadaye kulipa kwa awamu kiasi kilichobaki na kukamilisha deni hilo kufikia desemba 2019.
Taasisi nyingine zilizotembelewa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kuahidi kulipa madeni yao baada ya uhakiki ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) inayodaiwa bilioni 1.4, na EPZA milioni 200 ambapo kwa upande wake TBA tayari imeandaa utaratibu wa kulipa deni hilo kwa awamu na tayari milioni 40 zimetengwa wakati EPZA ilihidi kutoa mchanganuo wa jinsi itakavyolipa deni hilo wiki hii.
Juni 11, 2019 Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliitisha kikao cha Taasisi ambazo ni wadaiwa Sugu wa kodi ya Pango la Ardhi takriban 200 kwa kuwapa taarifa ya kulipa madeni yao sambamba na kuhakiki madeni hayo kabla ya hatua za kisheria hazijachukuliwa kwa watakaokaidi kulipa madeni hayo. Ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ilikuwa ni kuangalia taasisi zinazodaiwa zimekwama wapi kutekeleza agizo lililotolewa.
Social Plugin