Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Wizara ya Kilimo inaendelea na mkakati madhubuti wa kuwatambua wakulima wote nchini ili kuwa na ufahamu wa watu wanaopaswa kuhudumiwa kwa ajili ya pembejeo za kilimo.
Mkakati huo wa wizara wa kuwatambua wakulima nchini unahusisha usajili wa wakulima ili kubaini mahali wanapoishi, ukubwa wa mashamba yao na mazo wanayolima.
Hayo yamebainishwa jana tarehe 25 Julai 2019 na Mbunge la Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe Mhe Japhet Hasunga ambaye ni Waziri wa Kilimo wakati akizungumza kwenye mikutano ya hadhara katika kijiji cha Chizumbi, Ukwile, Chimbuya katika kata ya Isandula pamoja na Kijiji cha Ikomela, Isandula na Kilimampimbi vilivyopo kata ya Kilimampimbi wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa shughuli za maendeleo jimboni humo.
Alisema kuwa asilimia kubwa ya waTanzania wanawategemea wakulima katika kukamilisha mahitaji yao lakini wakulima hao hawatambuliki, hivyo mkakati wa utambuzi wa wakulima utaimarisha uwezekano wa kuwahudumia ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Mhe Hasunga pia amewaeleza wananchi hao lengo la serikali kuanzisha mradi mkubwa wa ujenzi wa treni ya kisasa itakayorahisisha huduma za kijamii ikiwemo usafirishaji wa mizigo yakiwemo mazao ya wakulima.
Pia amesema kuwa serikali inaendelea na mchakato wa kuwafikishia wananchi huduma bora ikiwemo upatikanaji wa umeme katika maeneo yote vijijini.
Kuhusu sekta ya Kilimo Mhe Hasunga amesema kuwa katika kipindi cha muda mrefu wakulima wamekuwa wakilima lakini matokeo yake wanapata hasara au kipato cha kujikimu hivyo ili kupata faida na tija ni wazi kuwa wakulima lazima wabadilishe mtazamo ili waweze kuwa na Kilimo chenye tija na kibiashara.
Alisema wizara yake imejipanga kutoa elimu bora kwa wakulima juu ya Kilimo ili kufuata taratibu za Kilimo bora zinazotolewa na wataalamu mbalimbali wa Kilimo katika vijiji.
Kadhalika Mhe Hasunga amesikitishwa na wananchi kutokula vizuri ilihali wao ndio wazalishaji wakubwa wa mazao ya mbogamboga na matunda.
"Ukienda mahospitalini watu wengi wanaoumwa ni wakulima, kwahiyo nawasihi wakulima mkizalisha chakula muwe wa kwanza kula vizuri halafu ziada ndio mkauze" Alisisitiza Mhe Hasunga
MWISHO
Social Plugin