Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma
Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya dola trilioni 1.4 zinapotea kila mwaka kwa njia ya rushwa barani Afrika.
Hayo yalisemwa Julai 11,2019 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dokta Damas Ndumbaro katika ufunguzi wa siku Maalum ya Mapambano dhidi ya rushwa kwa nchi za Umoja wa Afrika.
Dokta Ndumbaro amesema tathmini iliyotolewa na Umoja wa Afrika mwaka 2014 inaonesha kwamba zaidi ya Asilimia 25% ya GDP ya nchi za Afrika inapotea kila mwaka na jumla ya Dola bilioni 148 zinapotea kila mwaka kwa njia ya rushwa.
Aidha ,Dokta Ndumbaro amesema kutokana na ripoti inayohusu upotevu wa fedha na rasilimali iliyotoka Februari,2019[Illicit Finacial Flow Report for Africa]inaonesha kuwa Afrika inakadiriwa kupoteza kiasi cha Dola Bilioni 1.2 hadi kufikia Dola Trilioni 1.4 kwa Mwaka.
Hata hivyo Dokta Ndumbaro amesema Tanzania inaonekana kuongeza kiwango cha utawala bora kwa kupata alama hamsini na nane na nusu kwa mia moja [58.5/100 ]na kuwa nchi ya 14 kati ya nchi 54 kwa mwaka 2018 ikilinganisha na mwaka 2017 ambapo Tanzania ilipata alama hamsini na saba na nusu kwa mia moja[ 57.5/100] na kuwa nchi ya 17 katika bara la Afrika kwa mujibu wa ripoti ya MO Ibrahim Index Of African Governance[IIAG].
Dokta Ndumbaro ameendelea kusema kwa mujibu wa ripoti zinazotolewa na Transparency International [CPI]ilionesha kuwa ndani ya miaka mitatu[3]tangu 2015 hadi 2018 Tanzania imepanda hatua 18ambapo mwaka 2015 ilishika nafasi ya 117 kwa kupata asilimia 30% wakati mwaka 2018 imeshika nafasi ya 99 kati ya nchi 180 duniani kwa kupata alama 36 huku upande wa nchi za Afrika Mashariki ikishika nafasi ya pili ikitanguliwa na Rwnda.
Utafiti mwingine wa Taasisi ya ndani ya nchi REPOA [AFROBAROMETER],2017 inaonesha wananchi 7 kati ya 10 [71%] Ya waliohojiwa walisema ushiriki wa serikali katika mapambano dhidi ya rushwa ni nzuri ambapo imeongezeka kwa asilimia 37 ya kwenye matokeo yaliyotolewa mwaka 2014.
Katika hatua nyingine,matokeo ya utafiti uliofanywa na TWAWEZA Mwaka 2017 umebainisha asilimia 85% ya wananchi waliohojiwa walieleza kuwa rushwa imepungua ikilinganisha na asilimia 11% ya waliohojiwa mwaka 2014.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU hapa nchini Diwani Athuman amesema Tsh.Bilioni 86 ya Mishahara hewa zimeokolewa huku akiwataka wananchi kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Aidha ,Bw.Athuman amebainisha changamoto zinazoikabili TAKUKURU ikiwa ni pamoja na mashahidi kutotoa Ushahidi Mahakamani,na ufinyu wa bajeti.
Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali Prof.Juma Musa Assad amesema rushwa ni adui wa haki hivyo ni wajibu wa kila mmoja kujidhatiti katika mapambano dhidi ya rushwa huku pia akiiomba serikali kuongeza bajeti katika mapambano hayo.
Akifunga siku Maalum ya Mapambano dhidi ya rushwa kwa nchi za Umoja wa Afrika , Naibu Waziri wa ofisi ya Rais,Menejimenti ya utumishi wa Umma na utawala Bora Dokta Mary Mwanjelwa ametoa wito kwa watanzania kuwa askari katika mapambano dhidi ya rushwa huku pia akitoa rai kwa bodi ya Umoja wa Afrika ya Mashariki kwa udhihirisho kuwa siku ya mapambano dhidi ya Rushwa ni muhimu hivyo ni wajibu kila mmoja kushiriki kikamilifu.
Siku Maalum ya Mapambano dhidi ya rushwa kwa nchi za Umoja wa Afrika imeenda sambamba na kauli mbiu isemayo”Kuelekea kwenye Msimamo wa Pamoja wa Afrika kuhusu urejeshwaji wa Mali”ambapo kwa hapa Tanzania maadhimisho hayo yakifanyika ukumbi wa Pius Msekwa Bungeni jijini Dodoma huku wadau mbalimbali wakihusishwa ushiriki hasa vijana kwani asilimia 63% ya Watanzania ni Vijana.