Mahakama ya Wilaya ya Lindi imemuhukumu mkazi wa kata ya Rutamba, Issa Mpanyanje (51) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka 10.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu wa mahakama hiyo, Liliani Rugalabamo, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo mshitakiwa alipewa nafasi ya kujitetea ambapo aliiomba mahakama hiyo imuonee huruma kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza pia anayo familia akiwemo mke na watoto wanaomtegemea hivyo iwapo atapata adhabu kali itawafanya wakose huduma zake.
Hakimu Rugalabamo akitoa adhabu katika kesi hiyo namba 34/2019, kupitia vifungu 130 kifungu kidogo (1) na (2) (e) na 1321 kifungu kidogo Sheria sura ya 16 kama ilivyofanywa marejeo mwaka 2002 alisema amesikia maombi ya pande zote mbili,lakini kutokana na Sheria kumshika mikono, amemuhukumu kwenda jela miaka 30 na atakapomaliza adhabu yake amlipe mlalamikaji fidia ya Sh milioni mbili.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mwanasheria wa Serikali, Rabia Ramadhani kuwa mshitakiwa huku akitambua anachokifanya ni kosa, Aprili 14 mwaka huu maeneo ya mashambani bila huruma alimbaka mlalamikaji na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.
Inadaiwa mshitakiwa alipata mwanya huo baada ya kumshawishi mlalamikaji waende shambani akamsaidie kuvuna karanga na baada ya kufika huko alianza kumtomasa kisha kumbaka huku akimsisitiza kutomwambia mtu yeyote.
Hata hivyo kutokana na maumivu makali aliyokuwa akiyaona Mtoto huyo waliporejea Nyumbani alilazimika kukiuka maagizo aliyopewa na kumweleza mama yake ambapo naye alitoa taarifa kituo cha Polisi ambapo alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Social Plugin