Mkuu wa wilaya ya Kyela Claudi Kitta
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Jeromi Ngowi, amesema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kuweza kuwabaini wale wote waliohusika na kuvamia msafara wa Mkuu wa wilaya ya Kyela Claudi Kitta, katika Kijiji cha Mpunguti wilayani humo.
Kamanda Ngowi amesema kuwa msafara huo haukutekwa bali ulishambuliwa kwa mawe na kwamba Mkuu wa Wilaya na wenzake wako salama na hali ya usalama na utulivu imekwisharejea.
''DC na wenzake wako salama hali ya amani na utulivu imerejea mimi nipo eneo la tukio, kuna bwana amefariki kwenye uwanja wa mpira wananchi wakawa wanahisi mama yake mzazi amemuua kwa imani za kishirikina, maiti ilipotaka kuzikwa wakakataa wakamtaka mama yake amfufue" amesema Kamanda Ngowi.
Aidha Kamanda Ngowi ameongeza kuwa, "Hakuna mtu ambaye amelazwa wala kujeruhiwa, isipokuwa vurugu zilikuwa kubwa kidogo ila walijitahidi kutumia mbinu kujiokoa na sisi tuliwahi kufika na kuwasaidia, bado nipo hapa ili kufuatilia zaidi kujua waliohusika na vurugu hizo.".
Inaelezwa kuwa vurugu hizo zilianza juzi siku ya Agosti 27, 2019.
Chanzo - EATV
Social Plugin