Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HATIMA YA UBUNGE WA TUNDU LISSU KUJULIKANA LEO

Mahakama  Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo inatarajia kutoa uamuzi  endapo maombi yaliyowasilishwa na aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu  yanasifa ya kusikilizwa na mahakama hiyo na kama aliyefungua kwa niaba yake anayo mamlaka ya kufanya hivyo.



Uamuzi unatarajia kutolewa leo mbele ya Jaji Sirilius Matupa,baada ya kusikiliza sababu nane za kupinga maombi hayo ambayo wanadai hayajakizi vigezo vitano kati ya sita.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa Lissu, Peter Kibatala katika kupinga hoja za kutaka maombi ya mteja wake kutupwa  anadai  hoja za wajibu madai hazina mashiko na akaiomba mahakama izitupilie mbali.

Anadai hoja ya kutoambatanisha uamuzi wa Spika uliomvua ubunge Lissu, hilo si hitaji la lazima la kisheria.

Kibatala anadai kwa mujibu wa Kanuni ya  5 ya Mwenendo wa Mashauri ya Mapitio ya Maamuzi ya Mamlaka za Kiserikali, hakuna mahali ambapo panataja kuwa lazima kuambatanisha uamuzi unaolalamikiwa katika maombi ya marejeo ya uamuzi wa mamlaka za kiserikali.

Alisema kwa mujibu wa Kanuni ya 4 hata waliozitunga hawakuweka hilo kama hitaji la lazima kwa kuwa wakati mwingine uamuzi wa mamlaka za kiserikali hufanyika kwa maneno tu na kutekelezwa.

Kuhusu hoja alichokifanya Spika halikuwa tangazo, bali taarifa tu kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kuwa kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kiko wazi, Kibatala anasema alichokifanya kina uamuzi ndani yake.

Anadai Mwenyekiti wa NEC  hawezi kwenda bungeni kungalia nani hayuko bungeni, bila ruhusa ya Spika na kwa upande wa mamlaka ya kisheria kwa kaka wa Lissu, Alute Mughwai kufungua shauri hilo, Wakili Kibatala anadai  hoja hiyo si ya kisheria kwa kuwa ni hoja inayohitaji ushahidi.

Mawakili wa Serikali kwa upande wao kwa kuongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Clement Mashamba waliwasilisha hoja nane za kupinga maombi hayo wakidai hayajakidhi  vigezo vitano kati ya sita na aliyemwakilisha kufungua hana mamlaka ya kufanya hivyo, wanaomba yatupwe


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com