Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KASI YA MAENDELEO YA RAIS MAGUFULI KUSAIDIA KUIMARISHA SADC

Na Judith Mhina-Maelezo

Kasi ya Maendeleo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliyoionyesha katika kipindi cha miaka minne akiwa madarakani, itaamsha ustawi wa miradi ya kimkakati katika Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika –SADC.

Dhahiri, bila kificho kitendo cha kumkabidhi na kuwa Mwenyekiti wa SADC Rais Magufuli kitachochea ongezeko la shughuli za miradi mbalimbali ya kimkakati ya maendeleo, ambayo haikutegemewa na jamii ya Jumuiya SADC kama inaweza kutekelezwa na Tanzania na kuwa mfano wa kuigwa.

Mafanikio ya Rais Magufuli yameonekana waziwazi katika miradi mikubwa ya maendeleo, matukio kadhaa ya kitaifa na kimataifa, ambayo yamedhihirisha kuwa juhudi na mtazamo wa Rais Magufuli ni faraja na muelekeo mzuri wa kufanikisha maendeleo katika nchi wanachama wa- SADC.

Akitoa hotuba ya kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kusini Cyril Ramaphosa Rais Magufuli amesema”Katika kutekeleza mipango ya maendeleo na dira ya kufikia uchumi wakati ifikapo 2025, Tanzania inawakaribisha wawekezaji mbalimbali na kwa kuwa Afrika ya Kusini imepiga hatua kubwa katika Viwanda nawaaalika wafanyabiashara kuja kuwekeza katika Viwanda mbalimbali hudusan vya dawa na vifaa tiba, kuchakata madini na kwamba serikali iatatoa ushikiano  utakaohitajika”.

Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa sisi Tanzania tumeamua  kununua bidhaa kutoka Afrika ya Kusini, ambapo, hata pikipiki zinazotumika katika  mapokezi ya wajumbe kutoka nchi za SADC zimetoka Afrika ya Kusini. Amesisitiza Rais Magufuli.

Kama hiyo haitoshi, amemuomba Rais Ramaphosa kuongeza ushirikiano katika utalii hasa kwa kuwa wao wanapokea watalii takriban milioni 10 kwa mwaka ikilinganishwa na Tanzania inapokea watalii milioni 1.5 kwa mwaka. Katika hilo alitoa wito Afrika ya Kusini kuongeza safari za treni ya watalii na wawekezaji wake kuja kuwekeza katika hoteli  na fukwe za Tanzania, dhamira ambayo si kwa Afrika Kusini tu bali kwa nchi zote za SADC.

 Akiongea mara baada ya kuwasili nchini Zimbabwe mapema mwezi  Mei, Rais Magufuli amesema “Wakati umefika Jumuia ya Kimataifa kuiondolea nchi ya Zimbabwe vikwazo kwa kuwa vikwazo hivi vinaadhiri wananchi wanyonge wa Zimbabwe”

Aidha, Rais Magufuli amewaambia mabalozi wa nchi mbalimbali walioko Zimbabwe kuwa vikwazo hivi pamoja na kuwaadhiri Wazimbabwe pia, vinawaadhiri mabalozi na familia zenu mlioko hapa. Wakati umefika mliangalie hili na kuliondoa. Ili kila raia, aishiye Zimbabwe afurahie maisha mapya  na kuweza kushirikiana katika nyanja za uchumi kuongeza biashara na ushirikiano kati yetu.

Hakika Rais Magufuli amedhamiria kwa dhati kuleta maendeleo katika SADC, hakuna nchi  yeyote ya Afrika na dunia kwa ujumla iliyowahi kutamka nchi ya Zimbabwe iondolewe vikwazo kutoka kwa bwana wakubwa wa dunia. Hii inadhihirisha Rais Magufuli atachochea  ukuaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo, kuhakikisha ushirikiano na nchi za Kusini mwa Afrika na kuleta ustawi wa hali za maisha za wananchi wanyonge katika jumuiya.

Katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa ziara yake nchini Namibia Rais Magufuli alihakikisha anaelekeza kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara katika nchi za Kusini mwa Afrika ili kukuza zaidi ushirikiano ambao utawaletea maendeleo wananchi wa pande zote mbili

Akifungua msimu wa ununuzi wa tumbaku  nchini Malawi Rais Magufuli amesema “Wananchi walio wengi Barani Afrika wapo katika sekta ya kilimo, hapa Malawi nimeambiwa zao  la Tumbaku linachangia asilimia 80 ya ajira, asilimia 60 ya fedha za kigeni na asilimia 37 ya pato la Taifa”.

Uchumi wa nchi nyingi za Afrika zinategemea kilimo kinachochangia pato kubwa la Taifa  pia, ni sekta inayoajiri watu wengi katika nchi zetu, Tanzania inatoa ajira kwa asilimia 70, mali ghafi asilimia 60 asilimia 30 inachangia pato la Taifa  na huingiza asilimia 20 ya fedha za kigeni. Hii inadhibitisha kilimo ni sekta muhimu Barani Afrika. Amesema Rais Magufuli

Rais Magufuli aliongeza  na kusema “Nimeambiwa katika uzinduzi wa zao la Tumbaku Serikali imeweka njia mbili za ununuzi kwa njia ya mkataba au mnada na Serikali imweka bei elekezi lakini, niwaomba wanunuzi msisite kununua kwa bei ya juu  ili kuwapa motisha wakulima wa zao la tumbaku pia mzingatie ubora na msichafue tumbaku kwa lengo la kuongeza uzito”.

Hotuba hii dhahiri inaonesha nia  hakika unaona dhamira yake ya kuhakikisha wakulima wadogo wa tumbaku wananufaika na kilimo wanachokifanya  badala ya kunufaisha watu wa kati na wenye Viwanda bila kujali uwepo wa bei nzuri kwa wakulima. Rais Magufuli anatambua ukubwa wa kundi hili ambalo likiinuliwa uchumi wake maendeleo kwa nchi za SADC yataonekana.

Akionyesha Afrika ilivyo tegemezi kitu ambacho sio kizuri Rais Magufuli ameongeza kwa kusema kuwa, mazao ya chakula kwa sasa ni mazao ya biashara, kwa sasa Afrika wastani wa chakula kinachoingizwa kutoka nje kina gharama ya Bilioni 35 za Marekani. Ambapo soko la chakula Barani Afrika  ni Dola za Marekani 300.

Vilevile, dhamani ya soko la mazao ya chakula kwa soko la Afrika itafikia dola Trilioni 1 mwaka 2030. Tanzania mwaka 2019 imevuna mazao ya chakula ya ziada ikilinganishwa na Malawi, hivyo tunawakaribisha Malawi kuja kununua chakula kutoka Tanzania

Akielezea mikakati sita ya kukuza uchumi wa SADC, Rais Magufuli amesema “Ni lazima kuondoa vikwazo visivyo na maana kama ututuri wa kodi, kuondoa utitiri wa Taasisi zinazothibiti biashara, ili kuchochea kasi ya viwanda na maendeleo katika Jumuia ya SADC”.

Pia, Rais Magufuli amependekeza mambo kadhaa katika hotuba yake ya ufunguzi ya wiki ya Viwanda kama vile, tekinolojia ya viwanda, ambapo anahakika hii italeta mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda ndani ya Jumuiya ya SADC.

Akiangalia soko la SADC, Rais Magufuli amesema soko la watu milioni 350 na zaidi ni kubwa, idadi hii ya watu inatupa  jukumu la kujenga uchumi ndani ya Jumuiya husika. Pia, ubunifu ni kitu ambacho Rais amekiona ni muhimu katika Jumuiya, na kuhamasisha matumizi ya tekinolokia rahisi kwa kuwa rasilimali ya vijana wengi ipo, wenye vipaji katika sayansi na tekinolojia.

Aidha, uanzishwaji wa Viwanda vidogo vidogo kwa sababu hivyo ndivyo vinavyogusa watu wengi na kusisitiza viwanda hivi ndivyo vitakavyo inuka na kuwa viwanda vikubwa hapo baadaye. Hivyo ni lazima Jumuia iweke mazingira wezeshi katika kukuza sekta ya Viwanda. Amesisitiza Rais Magufuli.

Hii ikiwa ni pamoja na uwepo wa nishati ya umeme ya uhakika na bei nafuu, sekta ya usafiri na usafirishaji iwe rahisi na ya uhakika mfano reli ya kisasa (SGR), miundombinu ya barabara, usafiri wa anga wa uhakika.  Pia, kuruhusu idadi ya watu ndani ya Jumuia kutumia soko lililopo bila vikwazo kutoka nchi moja kwenda nyingine na kuhakikisha sekta binafsi inashiriki ipasavyo katika kujenga viwanda.

Rais Magufuli amesema”Tuhimize sekta binafsi, iache kulalamikia badala yake ipambane na changamoto zilizopo na kushirikiana na Serikali husika kuzitatua,  ili kutumia fursa zilizopo ipasavyo”.

Rais Magufuli ameonesha dhahiri nia yake ya kuhakikisha nchi za SADC zinafanya biashara, uwekezaji kuboresha miundombinu, kuongeza uzalishaji wa nishati ili kujenga Viwanda zaidi,  kuimarisha ulinzi na usalama na kulinda historia yetu kwa sasa na vizazi vijavyo ili kutambua tulipotoka, tulipo na tuendapo.

Pamoja na yote Rais Magufuli hakuacha ajenda yake ya lugha adhimu ya Kiswahili ambayo kwa hakika binafsi  nasema yeye ni shujaa wa kupigia chepuo lugha hii. Kila mtu ni shahidi hapa Tanzania kuwa tangu aingie madarakani amehakikisha anaitendea haki lugha hii kwa kuitumia katika shughuli  zake zote za Kitaifa na Kimataifa.

Ukiacha hafla zake chache kama pale alipoongea na wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Afrika ya Kusini  mwaka 2017 ziara ya Rais Jacob Zuma wakati huo, kwa sasa ni msataafu Ambapo aliomba radhi Watanzania kuwa atatumia lugha ya Kiingereza,  ili wafanyabiashara na wawekezaji waone umuhimu wa kumuelewa na kuwekeza nchini Tanzania.

Pamoja na mambo mengine muhimu, ziara hiyo ilizaa  makubaliano ya pamoja kuwa Afrika ya Kusini itaingiza  mitaala ya lugha a kiswahili katika shule zake za msingi na sekondari, hivyo kuwa na hitaji la  Waalimu kutoka nchini Tanzania. Ambapo Rais Magufuli aliwataka Waalimu kuchangamkia fursa hiyo.

Bila kificho tunajivunia lugha hii yenye  historia ya kujenga umoja na mshikamano, pia ni lugha ambayo inaasili  ya Afrika ambapo haimilikiwi na kabila lolote bali na Jumuia ya Afrika Mashariki na Tanzania ndio nyumbani kwake.

Ziara ya Rais Magufuli nchini Namibia mapema mwezi Mei mwaka huu,  imezaa kusainiwa kwa makubaliano ya pamoja ya kuwa lugha ya kishwahili iwe katika mitaala wa shule za msingi na sekondari  nchini Namibia. Hivyo nchi hiyo inahitaji kupatiwa waalimu wa lugha husika kutoka Tanzania.

Kama alivyoelezea  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Paramagamba Kabudi na ajenda ya kunadi lugha ya kishwahili  iwe moja wapo ya lugha rasmi za SADC . Hakika ni kielelezo kuwa ikitumika katika nchi wananchama wa SADC itafufua ari ya umoja na mshikamano wa kweli katika kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Ajenda hii ya matumizi ya lugha ya kiswahili iliyoibuliwa na kushikiwa bango na Rais Magufuli wakati alipohudhuria mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Afrika, mapema mwaka 2017. Alihutubia Mkutano huo kwa lugha ya kishwahili wakati wa ufunguzi wa jengo la kihistoria  la Julius Nyerere la Amani na Usalama Jijini Adiss Ababa Ethiopia kama Makao makuu ya Jumuia hiyo.

Juhudi hizo za Rais Magufuli  hatimaye zimeleta ajenda itakayowasilishwa leo katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa nchi za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Hivyo Lugha ya Kiswahili iwe lugha rasmi ya Mawasiliano SADC kama Kiingereza, Kifaransa na Kireno.

Nchi nyingine zilizoridhia kuingiza lugha ya Kiswahili katika mitaala ya shule zake za msingi na sekondari ni pamoja na Sudan Kusini, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikiwa ni pamoja na kuomba kupatiwa waalimu wa lugha hiyo kutoka Tanzania.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com