Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA AMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA UWEKEZAJI MKUBWA ALIOUFANYA KATIKA SEKTA YA AFYA

Na.Catherine Sungura, WAMJW-Dodoma

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa uwekezaji mkubwa aliouweka katika sekta ya afya nchini.

Dkt. Chaula ameyasema hayo jana wakati wa mahojiano na kituo cha runinga cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) wakati wa taarifa ya habari baada ya Mhe. Rais kutembelea Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyopo jijini Dar es Salaam.

Katika mahojiano hayo Dkt. Chaula alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano sio kwamba imewekeza tu kwa mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa serikali bali katika sekta yote ya afya kwa kuboresha huduma za afya kwa upande wa miundombinu, dawa, vifaa na vifaa tiba katika hospitali pamoja na taasisi zake.

Kwa upande kwa mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa serikali alisema kuwa serikali kupitia wizara ya afya imefanya jitihada kubwa za kusogeza huduma za mamlaka hiyo katika kanda zote nchini na hivi karibuni inatarajia kuwa na kanda nyingine jijini Dodoma.

“Sisi hapa kwa afrika mashariki, Tanzania tunaongoza kwa kuwa na mitambo ya uchunguzi ya kisasa vya kufanya utambuzi wa miili na tuna imani tutapokea hata vinasaba kutoka nchi za jirani pale panapotokea mkanganyiko hususani kwenye kesi za jinai,ajali,sumu,madawa ya kulevya pamoja na kemikali.

Dkt. Chaula alisema mitambo hiyo ya kisasa inatoa majibu ndani ya siku saba tofauti na zamani ambapo sampuli thelathini na tano zilichukua mwezi kuthibitisha ila kwa sasa wanachukua sampuli hadi mia mbili.

Hata hivyo katibu Mkuu huyo amewashauri watanzania kupenda na kujenga mazoea ya kutumia taasisi za serikali zilizopo nchini hususani mamlaka ya mkemia mkuu wa serikali pale panapotokea mkanganyiko kwa kisheria au utambuzi wa vinasaba mbalimbali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com