KOREA KASKAZINI YASEMA MAJARIBIO YA MAKOMBORA NI ONYO KWA MAREKANI


Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amesema majaribio ya makombora yaliyofanywa na nchi yake hapo jana, yalikuwa onyo kwa Korea Kusini na mshirika wake Marekani. 

Shirika la Habari la Korea Kaskazini KCNA limemnukuu Kim akisema kuwa onyo hilo ni jibu kwa mazoezi ya pamoja ya kijeshi yanayofanywa na vikosi vya Marekani na Korea Kusini. 

Awali, wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini ilisema kuwasili kwa nyambizi ya Marekani yenye silaha za nyuklia katika bandari ya Korea Kusini, ni sababu tosha ya nchi hiyo kuimarisha mpango wake wa silaha, na kuongeza kuwa sababu zinazotolewa na Marekani pamoja na Korea Kusini kutetea mazoezi yao ya pamoja, haziondoi azma yao ya uchokozi. 

Mapema jana Korea Kaskazini iliyarusha makombora mawili ya masafa ya kati kutoka mkoa wa Kusini wa Hwanghae, na makombora hayo yalisafiri umbali wa km 450 kabla ya kutua Baharini. 

Chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa, nchi hiyo hairuhusiwi kuyafanya majaribio hayo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post