Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LAAC YAIAGIZA OFISI YA CAG KUFANYA UKAGUZI NYANG’HWALE NDANI YA MIEZI 3 BAADA YA KUBAINIKA UBADHILIFU WA ZAIDI YA TSH.BILIONI 3


Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Kamati ya Bunge ya  kudumu ya Hesabu za serikali za Mitaa [LAAC]imeipa   muda wa  miezi 3 ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali [C.AG] Kwenda kufanya ukaguzi Maalum katika halmashauri ya  wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita baada Ya Kubainika Ubadhilifu wa zaidi ya Tsh.Bilioni 3.



Akizungumza  Mbele ya kamati hiyo leo  Agosti 22,2019  Bungeni Jiji Dodoma  ,iliyokutanisha  watumishi wa halmshauri ya  Nyang’hwale,watumishi  wa CAG ,Makamu Mwenyekiti wa LAAC , Abdallah Chikota amesema ofisi ya CAG imetoa hati mbaya kwa halmashauri  hiyo . 


Mhe.Chikota amesema katika halmashauri ya Wilaya Ya Nyang’hwale amesema baada ya ofisi ya CAG Kufanya ukaguzi wa ndani katika halmashauri hiyo kuna upotevu wa Zaidi ya Tsh.Bilioni 3,vitabu 50 vya ukusanyaji mapato havikuwasilishwa Kwa Mkaguzi  wa CAG,Kuna hati za Malipo [Voucher] zenye thamani ya Tsh.Bilioni 1,milioni 49, laki 1,40 elfu na 91  pamoja na uhamisho wa fedha Bilioni 1 na milioni 700 bila kuonesha shughuli zinakokwenda. 


Aidha Makamu Mwenyekiti huyo wa kamati amefafanua kuwa kuna zaidi ya Tsh.Milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya hazipo na kituo cha Afya hakijajengwa  huku kukiwa na Fedha za P4R  kwa Shule za Sekondari  Milioni  576 zikitumiwa nje ya Malengo yaliyokusudiwa ,Mradi wa Maji kulikuwa na salio la Tsh.Milioni 74.1 lakini benki inaonesha milioni 71.1 haipo  na hati za malipo kwenye mradi wa Maji  zenye thamani ya Tsh. Milioni  134.5 hazikuwasilishwa kwa wakaguzi. 


Naibu  Waziri wa TAMISEMI Mwita Waitara amesema jambo la ubadhilifu huo wao kama serikali limewafedhehesha sana huku akitoa wito kwa watendaji wapya kuwa waaminifu katika kuwahudumia Watanzania . 


Naye katibu tawala Mkoa Wa Geita Denis  Bandisa amesema ukaguzi  maalum wa CAG utaenda kuonesha utendaji kazi kwa halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale hata kwa viongozi wa sasa huku akibainisha kuwa wapo tayari kuipokea kamati ya CAG Kufanya ukaguzi huo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com