LORI LA MAFUTA LAANGUKA NA KUUA DEREVA KAGERA....WALIOCHOTA MAFUTA WAKAMATWA

Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog
Wakati bado Watanzania wakiendelea kuomboleza vifo vya  Watu 102 kufuatia ajali ya moto Morogoro ya lori la mafuta, baadhi ya Wananchi wa Kagera wamejitokeza kwa wingi kuchukua mafuta kwenye ajali ya Lori la mafuta lenye namba za usajili T456 CMY na tela lenye namba za usajili T861 CFT Scania lililoanguka jana majira ya saa 2 asubuhi Mali ya Lake Oil Trans eneo la Benako Ngara Mkoani Kagera.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani Kagera limewakamata  watu 8 wilayani Ngara, kwa tuhuma  za wizi wa mafuta katika gari  hilo lililopata ajali.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera  Revocatus Malimi, amesema pia wamekamata Lita 300 za mafuta, zilizoibiwa kwenye ajali hiyo.

"Baada ya kutokea ajali hiyo wananchi walianza kukimbilia eneo hilo la Beneko maarufu Machinjioni ambalo limekuwa na matukio mengi ya ajali wakaanza kuchota mafuta hayo bahati nzuri polisi waliwahi kufika eneo hilo na kufanikiwa kuwafukuza wananchi hao na tayari tunawashikilia watu 8",amesema.

Amesema kutokana na eneo hilo kuwa na mteremko mkali jeshi la polisi bado halijajua chanzo halisi cha ajali hiyo na huenda dereva Juma Msafiri (39)  alikuwa katika mwendo mkali na kusababisha gari imshinde na kupinduka na kusababisha kifo chake papo hapo.

Mara baada ya kutokea ajali hiyo, Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti alimuagiza mkuu wa jeshi la polisi mkoani Kagera  kufanya msako mkali wa kuwabaini wananchi katika eneo la Benako wilayani Ngara waliohusika katika zoezi la  kuchota mafuta au kujaribu kuchota mafuta kwenye lori la mafuta lililopata ajali  jana  asubuhi Agosti 25 2019,


‘’Hali hii inadhihirisha kwamba kuna baadhi ya wananchi hawajajifunza au hawataki kujifunza kutokana na ajali iliyotokea Agosti  10 mwaka huu huko mkoani Morogoro hivyo basi naagiza wahusika hao wakamatwe mara moja ili wafikishwe katika vyombo vya sheria",alisema Gaguti.

Mkuu wa mkoa ametumia fursa hiyo kutoa onyo kwa Wanakagera na Watanzania wote kwa ujumla kutambua kuwa ni vyema kujiepusha na matukio ambayo yanaweza kusababisha madhara makubwa katika taifa.

Wananchi wakiiba mafuta




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post