Mabalozi 42 wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali wamerejea Tanzania ili kushiriki Mkutano wa 39 wa Wakuu na Serikali katika Nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika(SADC) utakaofanyika Agosti 17 na 18, 2019, Dar es Salaam na kesho Agosti 14 watatembelea mradi wa ufuaji umeme wa Julius Nyerere Hydro Power Project (JNHPP) uliopo Rufiji Mkoani Pwani kujionea mradi huo unaotekelezwa na serikali kwa fedha za ndani ili kufanya diplomasia ya kiuchumi katika mataifa wanayotuwakilisha.
Akizungumza na wanahabari leo Jumanne Agosti 12, 2019 Jijini Dar es Salaam, Dk Abbas amesema ziara ya kutembelea mradi huo ni kukusanya taarifa zitakazowasaidia kujenga uwezo wakushawishi mazingira ya uwekezaji Tanzania.
“Kesho pia Tanzania tutampokea Rais wa Afrika Kusini, Cyill Ramaphoza kwa ajili ya kuanza ziara ya kitaifa ya siku tatu, itaanza kesho jioni hadi Agosti 16, pia atatembelea eneo la kihistoria Mazimbu, Morogoro lililotumika kusaidia ukombozi wa bara la Afrika.”
“Kwa hiyo viongozi wengi wa kusini mwa Afrika, si tu kwamba wanakuja katika mkutano ila wanarudi nyumbani na viongozi wote wamethibitisha kushiriki katika mkutano huo mkuu,” amesema Dk Abbas
Aidha amesema kuwa Agosti 15 mwaka huu Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa ataongoza mhadhara wa wazi ambapo ataeleza uzoefu wake juu ya jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kueleza kuwa mhadhara huo ni wa wazi kabisa na kila mmoja anaweza kushiriki ili kuweza kupata uzoefu kutoka kwa mzee Mkapa.
Mkutano huo wa wakuu wa nchi, viongozi wa serikali na wafalme unatarajiwa kuhitimishwa rasmi tarehe 17 na 18 mwaka huu.
Social Plugin