Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAJAMBAZI WAVAMIA MSIBA NA KUPORA FEDHA ZA KUNUNULIA JENEZA LA MAREHEMU

Familia moja katika eneo bunge la Kinangop, Kaunti ya Nyandarua,nchini Kenya iliyokuwa ikiomboleza ilipata majonzi zaidi baada ya kuvamiwa na majambazi walioiba Sh18,000 zilizokuwa zimetengewa ununuzi wa jeneza la kuzika marehemu. 

Kwa mujibu wa Taifa Leo, Rufa Thiga, mkewe na nduguye walivamiwa na majambazi sita mnamo Jumatano usiku, Julai, 27,2019 saa chache tu baada ya wageni waliofika kuomboleza kifo cha dada yao kuondoka.

Mke wa Thiga, Margaret Wambui na nduguye Benson Kigo walijeruhiwa kwenye kisa hicho. Thiga alisimulia jinsi alivyowasikia majambazi hao waking’ang’ana kuvunja lango kuu la kuingia boma lake na jinsi jaribio lake la kutorokea mlango wa nyuma lilivyogonga mwamba. 

“Nilipojaribu kutorokea mlango wa nyuma, watu wawili walinivamia kwa panga huku wengine wakiingia ndani ya nyumba na kumpiga mke wangu kwa silaha butu,” Thika alisema.

Simulizi hiyo inaendelea kwa kusema kuwa, baada ya hapo majambazi hao walimwagiza aingie ndani ya nyumba na awakabidhi pesa alizokuwa amekusanya kugharimia mazishi ya dadake.

 “Walinilazimisha kuingia ndani ya nyumba niwape pesa za matanga. Niliwapa KSh 18,000 ambazo zilikuwa zimetengewa ununuzi wa jeneza la marehemu,” akaongeza kusema. 

Wambui naye kwa masikitiko alisimulia jinsi majambazi hao walivyomfuata hadi kwenye bafu na kumpiga wakidai awape pesa.

“Walitishia kuua familia yote. Nilipata majeraha kwenye mikono, mgongo na kichwani,” akasema. Kigo naye alisema kuwa wezi hao walimlazimisha aingie ndani ya nyumba na akawapa KSh 3,000 ili kuyanusuru maisha yake.

 “Walinieleza kwamba walikuwa maafisa wa polisi kabla ya kunipiga kichwani na kuniamrisha nilale chini,” alisema. 

Haijulikani kufikia sasa ikiwa familia ya Thiga ilifanikiwa kupata pesa zingine na kuuzika mwili wa marehemu.
Via>>Tuko

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com