Akina mama katika Kaunti ya Kiambu nchini Kenya wameandamana wakililia haki yao baada ya kukosa kutimiziwa mahitaji yao ya ndoa na waume wao.
Akina mama hao Jumatano, Agosti 7,2019 waliandamana na kuteta kuwa kiu cha mapenzi kimezidi huku wazee wao wakiendelea kuwa magofu tu kitandani.
Waandamanaji hao walisema wengi wa wanaume huondoka nyumbani saa moja asubuhi kwenda kubugia kinywaji kwenye maeneo yaliyogeuka kuwa mwizi wa mahaba kaunti hiyo.
Susan Nyambura ambaye aliongoza maandamano hayo alisema hali ni mbaya sana katika maeneo ya Limuru mjini ambapo alidai kuna dada mmoja ambaye amewateka waume wao kwa kuwauzia pombe kwenye nyumba yake.
Aliongeza kuwa kwa sasa akina mama wana wasiwasi kwani wazee wao wameshindwa kushiriki tendo la ndoa.
"Wakifika kitandani atakuguza halafu anakuwacha kama hajakutosheleza. Sasa hata huwa hatutaki watuguse. Lakini tunashangaa tutazaa na kina nani?," alisema Nyambura.
"Mama Wengi wameachana na mabwana wao kwani hawawezi kazi kitandani, na hawaleti chakula nyumbani," aliongeza.
Kwenye maandamano yao, wakazi hao walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati na kuwasaidia kupigana na pombe haramu.
Walisema maeneo ambayo yameadhirika sana ni Limuru mjini, Nazareth, Ngarariga, Farmers Corner, Kwambira baadhi ya wengine.
Chanzo- Tuko