Mashine inayotumika kupima magonjwa ya ndani na kutambua taarifa mbalimbali katika mwili wa binadamu (Ultra sound) imeibiwa katika mazingira ya kutatanisha kwenye Hospitali ya mji wa Bariadi (Somanda) mkoani Simiyu.
Mashine hiyo inadaiwa kuibiwa pamoja na kifaa chake cha kudurufu picha (printer) ambapo ilikuwa maalumu kwa matumizi ya wodi mpya ya akina mama wajawazito na iliibiwa ikiwa kwenye wodi hiyo.
Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Mike Mabimbi, amekiri kuibiwa kwa mashine hiyo ambapo amesema hadi sasa bado haijapatikana.
Mabimbi amesema kuwa baada ya kutokea kwa tukio hilo waliweza kutoa taarifa jeshi la polisi, ambapo watu 17 wakiwemo wauguzi walikamatwa kwa ajili ya mahojiano.
“Ni kweli mashine hiyo ambayo ilitolewa na wadau wa maendeleo UNFPA kwa ajili ya wodi ya akina mama tu iliibiwa katika mazingira ya kutatinisha, tayari taarifa tulitoa na polisi wanaendelea na uchunguzi,” amesema.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Mwanaidi Churu, amesema mazingira ya kuibiwa kwa kifaa hicho yameendelea kuwa magumu kutokana na watoa huduma waliokuwepo wodini siku hiyo kila mmoja kudai hajui.
Credit: Mtanzania
Social Plugin