Jovither Kaijage, Ukerewe
Mkazi wa Kijiji cha Kagera wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, Celestin Masatu (39) amejichoma kisu tumboni, kujikata koromeo na kufa baada ya kumfanyia ukatili mkewe Jenifa Julias (30) wa kumchanachana mwilini na kisu, huku akiacha ujumbe akiomba msamaha kwa Rais John Magufuli kwa kitendo alichokifanya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi, saa 7.15 usiku, katika nyumba ya kulala wageni ya Emma iliyoko eneo la kata ya Nakatungulu mjini Nansio.
Alisema baada ya kumchoma visu mkewe na baadaye kujichoma kisu na kujikata koromeo, majeruhi hao wote walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya mjini Nansio usiku huo huo ili kupatiwa matibabu lakini Masatu alipoteza maisha asubuhi siku iliyofuata wakati mkewe akihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Kamanda huyo alisema kabla ya kujidhuru kwa kujichoma na kisu tumboni, kisha kukatakata utumbo wake na baadaye kolomeo, Masatu alimchoma visu tumboni na shingoni mkewe na kusababisha utumbo na mfuko wa kizazi uliokuwa na mtoto mchanga wa miezi miwili kutoka nje.
Alisema wawili hao, awali waliwahi kuishi pamoja kama mme na mke na walijaliwa kupata watoto wawili kabla ya mwanamke kuamua kuondoka na vifaa vya nyumbani na kwenda kuishi peke yake katika kijiji cha Bukongo.
Alisema hata hivyo katika siku za hivi karibuni walirejesha mahusiano yao ya ndoa na hadi siku hiyo ya tukio walikubaliana wakutane lakini kumbe mwanaume alikuwa na mpango wa kumdhuru mwenzake kwa sababu ya wivu wa mapenzi.
Baada ya Polisi kufanya upekuzi kwenye chumba walichofikia, mbali ya kupata kisu kilichotumika kuwadhuru na vitu vyao vingine kama nguo na viatu, pia lilipatikana daftari lenye maandishi yanayosadikika kuandikwa na Masatu akiomba msahama kwa Rais Magufuli kwa kosa alilolifanya na mgawanyo wa mali zake.
“Sehemu ya barua hiyo imeandikwa hivi, nanuku: ‘Naomba radhi kwa serikali inayoongozwa na Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kitendo nilitakachofanya kwa hiari yangu.’ Mmiliki wa nyumba ya kulala wageni ya Emma, Musiba Mayunga alisema alishitushwa na kelele za mwanamke akiomba msaada usiku wa manane na alipowataka wafungue mlango, mwanaume alikataa ndipo aliomba msaada wa uongozi wa kitongoji na Polisi.
Alisema kelele hizo ziliwaamusha wageni wengine waliofikia kwenye nyumba yake na ndio waliofanikiwa kuvunja mlango wa chumba na kuwatoa wanandoa hao wakiwa na majeraha.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Sokoni, Kata ya Nakatungulu, Celestin Mangwesa alisema baada ya kujulishwa na kufika eneo la tukio, alishuhudia mwanamke akitoka nje ya chumba utumbo ukiwa nje. Alisema mwanaume aligoma kutoka hadi Polisi walipowasili na kuamua kuingia ndani ndipo akatolewa akiwa amepoteza fahamu kutokana na majeraha makubwa aliyokuwanayo.
Social Plugin