Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga ACP Richard Abwao akionesha pikipiki ya mwendesha bodaboda Juma Nedadi mkazi wa Majengo Kahama Mjini aliyeuawa Agosti 8,2019 kisha pikipiki yake kuporwa na watu wasiojulikana Mjini Kahama.Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga limewakamata vijana wawili kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mwendesha bodaboda Juma Nedadi mkazi wa Majengo Kahama Mjini kisha kumpora pikipiki yake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Agosti 18,2019 ,Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga ACP Richard Abwao amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kutokana na msako wa jeshi la polisi katika kukabiliana na wahalifu na uhalifu mkoani Shinyanga.
Amemtaja mmoja wa watuhumiwa hao kuwa ni Daniel Anthony (26) ambaye amekamatwa akiwa na pikipiki ya marehemu katika eneo la Uyui Mkoani Tabora na baada ya kuhojiwa alieleza kuwa alipewa pikipiki hiyo na Answalata Semeni (23) ambaye ni fundi pikipiki mkazi wa Majengo Kahama ambaye pia anashikiliwa na jeshi la Polisi.
Kamanda Abwao amesema Juma Nedadi alikutwa akiwa ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na wauaji kutoweka na pikipiki yake yenye namba za usajili MC.841 CCG aina ya Honlg Agosti 8 mwaka huu katika eneo la shule ya msingi Malunga, Kata ya Malunga Wilayani Kahama.
Ameeleza mbinu iliyotumika kutekeleza uhalifu huo ni kumkodi dereva bodaboda huyo na kumpeleka katika eneo la giza lisilo na makazi ya watu kisha kumuua na kuiba pikipiki hiyo.
Na Annastazia Paul - Malunde1 blog
Social Plugin