Mawakili wa Serikali 15 wakiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Clement Mashamba wamewasilisha pingamizi katika Mahakama Kuu kupinga maombi ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kuhusu Ubunge wake.
Lissu amefunguka maombi Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya hati dharura, kupitia kwa Kaka yake Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge.
Dk. Mashamba amemueleza Jaji Sirilius Matupa kuwa mapingamizi hayo yana masuala manne ya msingi ikiwemo kuona kama mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikilizwa maombi hayo kama yalivyoletwa.
Pia amedai wameangalia kama mleta maombi ambaye ni Allute Mughwai ana uwezo wa kuleta maombi hayo na kama maombi hayo yameletwa kwenye mahakama yenye mamlaka.
Dk.Mashamba amedai wanaangalia kama nafuu zilizoombwa kwenye mahakama hiyo ni sahihi kuletwa mahakamani au la.
Katika pingamizi hizo, hoja ya kwanza iliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abubakari Mrisha amedai yapo mambo sita ya kuzingatia kwa mleta maombi ikiwemo kuhakikisha maombi yanaletwa ndani ya miezi sita baada ya maamuzi, mahakama kuona haja ya kusikiliza maombi hayo na maombi kuletwa kwa nia njema si kwa lengo la kupotosha au kwa manufaa binafsi.
“Kati ya hayo, jambo moja pekee kwamba maombi haya yako ndani ya muda lakini mengine yamekosekana katika maombi haya. Maombi haya hayakidhi kwa sababu hakuna maamuzi yoyote yaliyoambatanishwa katika maombi haya ili iweze kuyapitia kama kuna haja ya kuilazimisha mamlaka iliyotoa maamuzi kuyaondoa,” alidai Mrisha.
Pia amedai kuwa hakuna maamuzi yaliyoambatanishwa ili mahakamani iweze kuyapitia na kutoa uamuzi kama kwenye kesi ya aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Alidai kwa mujibu wa Kanuni za Bunge zinaelekeza Mbunge ambaye ataathiriwa na maamuzi anatakiwa kuwasilisha mapingamizi kwa Katibu wa Bunge ambaye atayawasilisha mapingamizi hayo kwa spika.
Mrisha alidai kisheria walipaswa kuambatanisha maamuzi wanayolalamikia na kwamba katika kiapo kilichoandaliwa na Mghwai walichoambatanisha ni nakala za magazeti ya Mwananchi na Nipashe ambayo kimsingi hawawezi kuyaita maamuzi.
Katika mapingamizi mengine, Wakili wa Serikali, Lucas Malunde alidai alichokifanya Spika ni kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa NEC juu ya uwepo wa nafasi ya wazi ya kiti cha Mbunge kwa sababu hakuwepo na hatekelezi majukumu ndani ya Bunge.
Malunde alidai taarifa hiyo ilitangazwa kwenye gazeti la serikali hivyo hakutoa tamko la kumvua ubunge na kwamba Lissu hakujiudhuru wala hajafa.
“Hakuna mahali Spika alitoa tamko yeye alitoa taarifa ambayo inapopelekwa gazeti la serikali inakuwa mali ya serikali inayosambazwa na mtu yoyote anaweza kuipata akihitaji,” alidai Malunde.
Alidai maamuzi ya kutostahili kuendelea na ubunge hayatolewi na spika kwani katiba inaelekeza Mbunge atakosa sifa ya kuendelea kuwa kwenye nafasi hiyo endapo atakosa kuhudhuria vikao vitatu vya bunge bila ruhusa ya Spika.
Wakili wa Serikali Mkuu, George Mandepo amedai sheria inaruhusu madai kufunguliwa na mtu binafsi au muwakilishi ambaye ana nguvu kisheria kwa hivyo, maombi yaliyopo mahakamani yamewasilishwa na Lissu kupitia mwakilishi wake ambaye ni Mghwai.
Alidai katika kuomba ridhaa ya kuwasilisha maombi yanatakiwa kusainiwa na muombaji au muwakilishi wake pamoja na kuambatanisha hati ya kiapo na muhuri wa wakili.
“Katika maombi haya yanaonesha kuwa Julai 9, mwaka huu Lissu alisaini kiapo hicho akiwa nchini Ubelgiji na muhuri wa wakili Sadolf Magai alisaini kwa anuani ya Dar es Salaam,” alidai Mandepo.
Alidai ipo sheria inayosimamia maombi inayoeleza kiapo kinatakiwa kutolewa mbele ya msimamizi wako.
Mandepo alidai kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria za Tanzania kwa sababu kiapo kilichowasilishwa kimesainiwa na muhuri wa Tanzania wakati kiapo kilisainiwa nchini Ubelgiji hivyo, sio halali na maombi yaliyowasilishwa sio halali.
Alidai wanashangaa Julai 9, mwaka huu siku ambayo kiapo kiliandaliwa huko Ubelgiji hakioneshi ni kwa namna gani kilifika jijini Arusha hivyo si kiapo cha kweli.
“Kiapo hiki kimebeba uongo kwa sababu moja wakili Sadolf hajaleta hati ya kiapo mahakamani wala maelezo ya kudhibitisha kwamba alikwenda Ubelgiji na hakuna kumbukumbu kwamba wakili huyo aliithinishwa kufanya kazi nchini Ubelgiji wakati aliapishwa na Jaji wa Tanzania,” alidai.
Kutoka na hoja hizo, aliomba mahakama iyatupe maombi kwani pamoja na mambo mengine aliyoyaleta, hana sifa ya kufanya hivyo.
Jaji Matupa jana alitakiwa kusikiliza maombi ya zuio la muda la kuapishwa kwa Mbunge Mteule, Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu na maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Tundu Lissu lakini haikuwezekana baada ya Jamhuri kuwasilisha pingamizi la awali.
Maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge yalifunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa zamani wa Jimbo la Singida Mashariki, Lissu kupitia mawakili wake.
Amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Wakili Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.
Jaji Matupa jana alitakiwa kusikiliza maombi ya zuio la muda la kuapishwa kwa Mbunge Mteule, Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu na maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Tundu Lissu lakini haikuwezekana baada ya Jamhuri kuwasilisha pingamizi la awali.
Maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge yalifunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa zamani wa Jimbo la Singida Mashariki, Lissu kupitia mawakili wake.
Amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Wakili Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.
Social Plugin