Na Issa Mtuwa “WM” Nachingwea Mtwara
Mgogoro ulio dumu kwa muda mrefu kuhusu mpaka wa uchimbaji madini uliohusisha eneo (leseni) moja kwenye ardhi ya halmashauri za wilaya mbili ya Nachingwea na Liwale kila upande ukiwa na wachimbaji wadogo umetatuliwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo tarehe 15/08/2019 mara baada ya kufanya ziara katika eneo hilo na kufanya mkutano na wachimbaji wadogo wa pande zote mbili na viongozi wa kuu wa wilaya zote mbili.
Mgogoro huo wa mpaka na leseni umedumu kwa muda mrefu ukiwa na vyanzo viwili vikuu vya mgogoro. Moja, mgogoro wa eneo ambalo wachimbaji wadogo wananchimba hivi sasa wamedai eneo hilo lilikuwa la Omar Said Kojogo ambae kwa mujibu wa wachimbaji wadogo walimlipa fidia ndugu Kojogi ili eneo hilo limilikishwe kwa jumuia ya wachimbajio wadogo lakini bado walikuwa hawajapatiwa leseni hiyo kama wamiliki wapya.
“Mhe. Naibu Waziri tatizo la mgogoro wa leseni hapa bado haujatatuliwa kwa kuwa sisi wenyewe wanaaporo tulichangishana na kumpa Omar Said Kojogo Tsh. 2,852,000/= ili leseni hiyo iwe ya wanaaporo (Wachimbaji wadogo) lakini mpaka leo hatujapatiwa” alisema Machui Bausi.
Chanzo cha pili cha mgogoro huo ni mgao wa mapato yanayopatikana katika eneo hilo. Kila halmashauri inataka ichukuwe mapato kitu ambacho kilikuwa kinaleta mvutano nani anastahili kwa kuwa leseni ya eneo hilo ipo katika halmashauri zote mbili. za Nachingwea na Liwale zote za mkoa wa Lindi.
Aidha, changamoto nyingine ambayo wachimbaji wadogo wamemwambia Naibu Waziri ni tatizo la soko la kuuzia madini ambapo wamemuomba Naibu Waziri kuwasongezea soko la madini katika eneo hilo ili kuwaondolea ushawishi wa kutorosha na kwenda kutafuta soko kwingine na ili mapato ya serikali yasipotee.
“Mhe. Naibu Waziri sisi hapa kiliochetu ni soko, hapa tulipo hata ukitaka kuuza madini lazima uende Ruangwa au Tunduru umbali uliopo ni mkubwa kufika huko. Na soko kubwa la Madini ya vito ni Tunduru, kwa hiyo ili mapato ya serikali yasipoteee tunaomba soko liwe hapa hapa sisi tuuze madini yetu na watu wa TRA wawepo ili tukiuza tuu serikali inachukuwa chake hapo hapo” alisema Ijumaa Iddi mwenyekiti wa wachimbaji wadogo katika eneo hilo.
Katika kupatia majibu hoja zote zilizo wasilishwa, Naibu Waziri alianza kwa kusema.
“Mimi na waziri wangu Biteko iwe mchana iwe usiku, tutafika mahali popote ili kuhakikisha serikali inapata mapato kupitia madini, hivyo uwepo wangu hapa ni kwa sababu hiyo na ili pesa hiyo ipatikane lazima migogoro na hizi kero lazima zimalizwe ili mchimbe, muuze na kisha mlipe mapato ya serikali” alisema Nyongo.
Katika kujibu hoja, Naibu Waziri alianza kwa msimamisha Kaimu Afisa Madini Mkazi mkoa wa Lindi Mhandisi Iddi atoe ufafanuzi kuhusu leseni na umiliki wa eneo hilo.
“Mhe. Naibu Waziri, kwanza kabisa niseme eneo hili lina leseni halali inayo milikiiwa na ndugu Omar Said Kojogo anae miliki kihalali kwa leseni Na. PML 36821 Southern Zone ya Tshs. 1,937,000. Na kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 hairuhusu kutoa leseni kwenye eneo moja ambalo teyari ilishatolewa na mahali hapa palishatolewa leseni kama nilivyosema, na kama itakuwa hivyo mlabda kwa kesi maalum, hata hivyo suala hili lilishashugulikiwa na muda si mrefu leseni yao itakuwa teyari” alisema Mhandisi Idd Msikozi.
Kuhusu kilio cha masoko, Naibu waziri alisema kwanza anawashukuru wachimbaji hao kwa kitendo chao cha kulilia soko ili madini yao yakauzwe kwenye masoko rasmi. Amesema serikali imetoa agizo kila mkoa uwe na soko la madini ili serikali ipate fedha za kutosha kupitia madini ili fedha hizo zikatumike kwenye shuguli nyingine za maendeleo.
Amesema mpango wa sasa wa wizara ni kuhakikisha kuwa kuna vituo vya kununulia madini kwenye maeneo ya wachimbaji ili wanaporo wasitembee mwendo mrefu kufuata soko.
“Ndugu zangu wanaaporo, kiliochenu kuhusu soko kimenigusa sanaa, na sisi kama wizara ndio kitu ambacho tunakisisitiza kila mahali, kwa hiyo hapa hapa naagiza Afisa Madini Mkoa na Uongozi wa Wilaya kaeni chini kwa haraka mjadili ili kituo cha kununulia madini hapa kianzishwe mara moja na serikali ianze kukusanya mapato yake”. Aliongeza Nyongo.
Baada ya kutolea majibu ya hoja za wachimbaji hao, Naibu waziri pia aliwaagiza wachimbaji kuanzisha mfuko wa mahafa na dharula ili uwezo kuwasaidia mara miongoni mwao anapopatwa na tatizo ahudumiwe kwa huduma ya awali huku akisubiri utaratibu binafsi wa kutatua tatizo lake.
Kwa upande mwingine Nyongo ameuagiza uongozi wa Wilaya zote mbili ukae pamoja na kuweka utaratibu utakao wezesha kuwa na kituo cha kutolea huduma ya kwanza kwa maana pawe na “Nurse” kwenye eneo hilo kwa utaratibu watakao ukubaliana. Aidha, halmashauri hizo ziweke vyoo maeneo hayo kwa kuwa wachimbaji hao wanalipa fedha serikalini hivyo wanastahili huduma hiyo.
Wakati huo huo Naibu Waziri amewapongeza viongozi wa Wilaya zote mbili kwa jitihada zao za kutatua mgogoro huo awali kabla hajafika hasa katika kukubaliana namna kukusanya mapato ya kila upande kwani mapato yote yanakwenda kwenye mfuko mmoja wa serikali.
Kwa upande wao viongozi wa wilaya ya Nachingwea Katibu Tawala Husna Sekibobo na Mkuu wa Wilaya ya Liwale Sarah Chiwamba kwa pamoja walimshukuru Naibu Waziri kwa kufika katika eneo hilo na kujione hali halisi kutoa majibu ya moja kwa moja ya hoja zilizo wasilishwa na waliahidi maelekezo na maagizo yake watayatekelezwa.
Ziara ya Naibu Waziri ilikuwa ya kukamilisha ratiba ya ziara ya Waziri wa Madini Doto Biteko aliesitisha ziara yake mkoani humo na kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya majukumu mengine.
Social Plugin