Mkulima wa Muhogo akimweleza jambo Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala
Na Rhoda Ezekiel Malunde1 blog
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala, amewataka wafanya biashara wa zao la muhogo kuacha tabia ya kuwaibia wakulima kwa kwenda kununulia shambani mihogo bila kutumia mzani akionya kuwa watakaobainika wananunua zao hilo bila kutumia mzani watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Maagizo hayo ameyatoa leo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima wa kata ya Kasanda wilayani Kakonko, ambapo wakulima hao walisema wanalazimika kuuza zao hilo kwa gunia kwa shilingi 12,000/=.
Ndagala amewaagiza wafanya biashara wote kutumia mizani kupima zao hilo ili kuepuka kuwaibia wakulima, wakulima wengi wilayani Kakonko wanategemea zao la muhogo kuwapitia kipato na kuinua hali zao za uchumi.
"Kuanzia leo ni marufuku kwa mkulima yeyote kuuza mazao shambani, kwa kuwa itakuwa vigumu kuwabaini wafanyabiashara wanaowaibia wakulima kwa kutokutumia mizani; hata hivyo niwaombe tutayarishe zao hilo kwa ubora kwa kukausha juu ya turubai au vichanja ili kuwavutia wanunuzi kwa kununua kwa bei nzuri.
Niwatake wafanyabiashara kuacha tabia ya kuwanyonya wakulima kwa kununua kwa bei ya chini wakati ninyi mnakwenda kuuza na kupata faida zaidi", alisema Mkuu huyo.
Aidha aliwataka wakulima kuunda vikundi na kuweza kupatia mikopo na serikali pamoja na mashirika ilikuanzisha viwanda, waweze kuyaongezea thamani ya mazao hayo na kuuza katika masoko ya nje katika nchi za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako zao hilo linahitajika sana maeneo hayo.
Pia aliwaagiza maafisa biashara wa wilaya na watendaji wa vijiji kufuatilia na kuhakisha kuwa wanunuzi wa zao hilo na mazao mengine wanatumia mizani na iliyohakikiwa na wakala wa vipimo.
Mkazi wa Kasanda, Anthony Mlengera alisema wao kama wakulima wanalazimika kuuzia shambani kwa kuwa kwa sasa zao hilo halina soko hivyo waliiomba serikali kuwatafutia soko la zao hilo ili waweze kuuza kwa bei nzuri ambapo hapo awali bei ya zao hilo lilikuwa zaidi ya shilingi 500.
Alisema walihamasishwa sana na maafisa kilimo kulima zao hilo kwa kuwa bei yake ilikuwa nzuri na wamelima zaidi. Na kuelezwa kwamba zao la muhogo linahitajika nchini China na sasa hakuna wanaokuja kuchukua zao hilo mbali ya wafanya biashara kutoka nchi jirani kuja kununua kwa bei ya chini sana hivyo kuwaumiza wakulima.
Naye Kagoma Hamisi mkulima katika Kijiji cha kabingo alisema serikali ikitaka kumaliza tatizo hilo la wakulima kuibiwa na kuuza kwa bei ya chini, kuwepo na bei elekezi ya zao hilo kwa maeneo yote yanayolima muhogo kama ilivyo kwa mazao mengine kama vile pamba ili kuondoa changamoto ya mkulima kuibiwa na kuuza kwa bei ya chini.
Social Plugin