Na Asha Shaban - Malunde1 blog Mara
Mtu mmoja ambae jina lake halijafahamika amefariki dunia kwa kupigwa na mshale sehemu zake za siri na wengine wawili kujeruhiwa kwa mishale hiyo na mtuhumiwa ajulikanae kwa jina la Mtunde kwa kosa la kunyimwa pombe kwenye sherehe huko katika kitongoji cha Nyamakendo wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa polisi mkoa wa Mara Juma Ndaki alisema tukio hilo lilitokea Julai 28,2019 majira ya saa 2 usiku katika kitongoji hicho ambapo mtuhumiwa alitenda kosa hilo wakati wa sherehe ya ugeni kwa baba yake wa kufikia akiwa anadai kupewa pombe.
Alisema kabla ya kutokea kwa tukio hilo mtuhumiwa alishapewa pombe aina ya bia chupa mbili na kudai kuongezewa pombe hizo ndipo baba mlezi ajulikanae kwa jina Juma Joseph alipomkatalia na kumwambia pombe zilizobakia ni za wageni.
Aliongeza kusema kuwa "Baada ya kujibiwa hivyo mtuhumiwa huyo alichukia na kuanza kumfokea baba yake huyo kuwa ni mchoyo huku akisistiza kuwa kabila la kisukuma ni la uchoyo na kumtolea kauli ya kuwa utaona lakini kauli hiyo baba hakuiwekea maanani.
"Kijana huyo aliondoka na kisha kurejea majira hayo ya saa mbili usiku na kukuta watu wakiwa wamekaa wakiendelea na sherehe ndipo alipoanza kuirusha mishale hiyo kwa kutumia upinde na kufanikisha kumuua mwanamke huyo mmoja na kujeruhi wengine wawili",alieleza.
Alisema waliojeruhiwa katika tukio hilo ni baba mlezi wa kijana huyo Juma Joseph ambaye alipigwa mshale katika mguu wake wa kushoto mwingine aliyejeruhiwa alifahamika kwa jina moja la Meng'anyi (74),mkulima alijeruhiwa katika titi lake la kushoto na majeruhi wote wamelazwa katika hospitali ya DDH ya Wilayani Serengeti mkoni Mara.
Aidha kamanda ndaki alisema mtuhumiwa alipotenda kosa hilo alikimbilia nchi jirani ya Kenya ambapo alisema juhudi za kumsaka zinaendelea kwa kushirikiana na askari wa nchi jirani ya Kenya na pindi atakapokamatwa atafikishwa katika vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake na iwe fundisho kwa watu wengine.
Social Plugin