Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam nchini Tanzania, imemhukumu mwanafunzi wa mwaka wa pili, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Julius Warioba (23) kulipa faini ya Sh5 milioni au kwenda jela mwaka mmoja.
Ni baada ya kukiri shtaka la kuchapisha maudhui katika Mtandao bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Warioba ambaye ni mshereheshaji (MC) anadaiwa kuchapisha maudhui kupitia Televisheni ya mtandaoni inayojulikana kwa jina Mc Warioba, bila kuwa na kibali kutoka TCRA wakati wakijua kuwa ni kinyume cha sheria ya Mtandao.
Mbali na faini, Mahakama hiyo, imetaifisha kompyuta aina ya Apple na simu ya mkononi aina ya Iphone ambavyo vilitumika katika kuchapisha maudhui hayo.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo amefanikiwa kulipa faini na hivyo kukwepa kifungo.
Hukumu hiyo imetolewa jana Jumatatu Agosti 26, 2019 Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Janeth Mtega baada ya mshtakiwa kutiwa hatiani.
Social Plugin