Naibu waziri wa maji, Juma Aweso ameagiza kukamatwa na kufukuzwa kazi watumishi watatu wa mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ( Muwasa) mkoani Mara kwa tuhuma za kuhujumu mamlaka hiyo.
Aweso alitoa agizo hilo mjini Musoma mkoani Mara jana Jumanne Agosti 6, 2019 wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa idara hiyo baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi ya maji katika manispaa ya Musoma.
Watumishi hao ambao baada ya agizo hilo waliwekwa chini ya ulinzi na polisi ni pamoja Meshack Marco, Ramadhan Evarist na Jonas Paschal.
Aweso alisema katika ukaguzi huo amebaini watumishi hao pamoja na wengine ambao bado hawajatambuliwa wamekuwa na tabia ya kuwaunganishia maji wateja na kukusanya ankara za maji kila mwezi kinyume cha utaratibu.
"Nimekwenda Nyakato kuna mama alitoa Sh210,000 ili aunganishiwe maji na pesa hizo alipewa mtumishi anaitwa Rosta Kusaga lakini pesa iliyopelekwa kwenye mamlaka ni Sh 23,000 tu," alisema Aweso
Alisema mbali na vitendo hivyo lakini watumishi hao wamekuwa vinara wa kutunga uongo ili uongozi wa mamlaka hiyo uonekane mbaya jambo ambalo alisema sio zuri kwa maslahi ya wakazi wa Musoma wanaotegemea mamlaka hiyo.
Alitolea mfano wa barua iliyoandikwa kwa pamoja na watumishi hao kwenda kwa waziri wa maji huku wakidai mkurugenzi wa mamlaka hiyo amekuwa akitoa ajira kwa misingi ya ukabila wakidai robo tatu ya watumishi wa mamlaka hiyo ni kabila moja na mkurugenzi huyo jambo ambalo alisema kutokana na uchunguzi alioufanya amegundua kuwa sio kweli.
"Kuhusu suala la watumishi na maslahi yao nimeagiza muhusika wa masuala ya watumishi kutoka wizarani aje hapa aweze kupitia malalamiko ya watumishi ili kila mmoja aweze kupata stahiki zake maana hatutaki kumuonea mtu ila pia hatuko tayari kumvumilia mtu anayehujumu mamlaka," alisema Aweso
Social Plugin