Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI AMALIZA MGOGORO WA ARDHI ULIODUMU KWA MIAKA 10 MKOANI MOROGORO


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametatua mgogoro wa ardhi uliodumu  kwa muda wa miaka 10  kati ya wanakijiji wa Kumbulu na  msitu wa Hifadhi ya Kumbulu unaosimamiwa na Halmashauri ya wilaya ya  Gairo kwa kushirikiana na  Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Mhe. Kanyasu amesema mgogoro huo wa ardhi  ulianza  mwaka 2009 baada ya kijiji hicho kupanga matumizi bora ya ardhi ambapo kutokana na baadhi ya  viongozi wa kijiji hicho kutokuridhia uamuzi huo na kuanza kuwachochea wananchi kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya msitu huo.

Kufuatia hali hiyo, Kanyasu ameagiza  kamati iliyosheheni wataalam mbalimbali ambayo ilikwisha undwa na wilaya ya Gairo igawe upya maeneo hayo kwa kuzingatia idadi ya watu katika kijiji hicho  kwa kuongeza eneo la kilimo kutoka ekari 1,000 hadi ekari  2,314 kwa kulimega eneo la msitu wa hifadhi wenye ukubwa wa ekari 5,500 hadi 5000 ili eneo hilo  litumike kwa ajili ya kilimo.

Aidha, Kanyasu ameagiza eneo la malisho lipunguzwe kutoka ekari 1,641 hadi ekari 1,000 ili ekari 641 iweze kutumika kwa ajili ya  kilimo.

Ameyatoa maagizo hayo wakati akizungumza na wananchi wa  kijiji cha Kumbulu  wilayani  Gairo katika mkoa wa  Morogoro.

Kutokana na  malalamiko hayo ya wananchi, Kanyasu aliwaeleza wananchi hao kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi  uliofanyika  mwaka 2008 ulibainika kuwa na  kasoro kwa vile  baadhi ya  wananchi walichukua ardhi kubwa na kuna wengine  walichukua na kuiuza na kuna wengine walihamia kijijini hapo kwa ajili ya kutafuta ardhi.

Akizungumzia kuhusu ugawaji  huo wa ardhi kwa kila kaya,  Mhe. Kanyasu amesema  kijiji hicho  kina  kaya 642 hivyo kila kaya itagawiwa   ekari mbili na hivyo kufanya  jumla ya ekari 1,284 kati ya ekari 2,314.

Awali,   mpango huo wa matumizi bora ya ardhi  ulitenga eneo la misitu wa hifadhi ekari 5,500,  eneo la kilimo ekari 1,000 pamoja na eneo la malisho la ukubwa wa  ekari 1, 600  lakini bado viongozi wa kijiji hicho licha ya kushirikishwa katika mpango  huo  waliendelea kuwahamasisha wananchi kuvamia misitu huo kwa madai kuwa hawayatambui maamuzi hayo.

Aidha, Mhe. Kanyasu amesema kwa vile Msitu huo wa Hifadhi unapakana na vijiji vitatu ni vyema na vijiji viwili mbali na kijiji cha Kumbulu kama navyo vina  uhitaji ya ardhi viwasilishe maombi yao ili kupunguza migogoro.

Katika hatua nyingine, Mhe, Kanyasu amezionya kaya hizo zitakazopata ardhi ziendeleze ardhi hiyo la sivyo zitanyang’anywa.

Pia, Kanyasu amevionya vikundi vya watu wenye maslahi binafasi  ndani ya kijiji hicho viache  tabia ya kuchochea migogoro ya ardhi la sivyo Serikali haitasita kuvichukulia hatua  kali za kisheria.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe Amewataka wananchi hao kutoa ushirikiano kwa Kamati hiyo wakati itakapokuwa ikitekeleza majukumu yake ili kila kaya iweze kupata ardhi kwa ajili ya kilimo

‘’Lazima mpate ardhi ya kilimo lakini ni muhimu pia kutunza miti iliyopo kwa vile bila miti hakuna kilimo kwa sababu miti inasidia kuleta mvua. Alisisitiza Mchembe

Naye, Mbunge wa Gairo, Ahmed  Shabiby amewataka wananchi hao wakati wakisubili kugawiwa maeneo kwa ajili ya kilimo wajiepushe na ukataji miti ovyo katika msitu wa Hifadhi ya Kumbulu.

‘’ Kwa wale wanaotaka kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa kwa ajili ya kuupeleka sokoni ni lazima mfuate sheria, hata ukitaka kuukata miti uliopo nyumbani kwako lazima uombe kibali kwa mamlaka inayohusika.’’ Alisisitiza  Shabiby


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com