Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAUME WAPANGA FOLENI KUNUNUA NGONO MWAKITOLYO.... ' KUCHEMSHA MASHINE'...DED AAGIZWA KUCHUKUA HATUA

Na Suleiman Abeid, Shinyanga
Mkurugenzi mtendaji katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba ameagizwa kuchukua hatua za haraka kuzuia vitendo vya uasherati vinavyofanywa na baadhi ya wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili yao katika kata ya Mwakitolyo wilayani humo.


Agizo hilo limetolewa mapema wiki hii katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga baada ya kutolewa kwa taarifa ya kukithiri kwa biashara ya wanawake wanaojiuza kiasi cha wanaume kupanga foleni wakisubiri kupatiwa huduma.

Taarifa hiyo iliyotolewa na mmoja wa madiwani iliwashitua madiwani wengine ambao walisema iwapo hali hiyo haitadhibitiwa haraka ipo hatari ya kuongezeka kwa kasi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI miongoni mwa wakazi wa wilaya hiyo na mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.

“Mheshimiwa mwenyekiti, binafsi nilipopata taarifa hii mimi mwenyewe niliamua kwenda Mwakitolyo kujiridhisha, na kweli nilichokikuta hakikunifurahisha, nilishuhudia mwenyewe katika nyumba zilizopangwa na wanawake hao kuna foleni za vijana wa kiume wengi wakisubiri huduma,”

“Niliuliza kuna biashara gani inayofanyika, jibu lilinishitua, ilibidi na mimi nipange foleni nikaone kule ndani kama kweli biashara hiyo ndiyo inayofanyika, lakini hata kabla sijaingia ndani nilishangaa kuona watu wanagonga milango wakisema, muda, muda, dakika zimekwisha tupishe na sisi,” alieleza diwani Isack Sengerema.

Akifafanua Sengerema ambaye ni diwani wa kata ya Iselamagazi, alisema biashara hiyo imekuwa ikifanyika wakati wote bila kujali muda wa kazi ambapo vijana wengi wafanyabiashara na wachimbaji madini ya dhahabu katika kata hiyo wamebuni msemo wa kwenda “kuchemsha mashine.”

Kwa upande wake Mbunge wa viti maalumu, Azza Hilal alisema yeye binafsi kama mwanamke amesikitishwa na hali hiyo na kushauri kuchukuliwa kwa hatua za haraka kuwadhibiti wanawake ambao wameamua kufanya biashara hiyo chafu.

“Taarifa hii imenisikitisha sana kama mama, ninachoshauri tuchukue hatua haraka, na nafikiri tuangalie uwezekano wa kuwapatia mikopo wanawake wanaofanya biashara hiyo,”


"Baada ya kutolewa taarifa ya matukio yanayoendelea Mwakitolyo, namshauri Mkurugenzi na mwenyekiti wa halmashauri..Mimi pamoja na madiwani wanawake twende tukaongee na hao wasichana wanaofanya biashara ya kuuza miili yao huko Mwakitolyo,tuwaulize wanataka kufanya nini kabla ya kuwapa mikopo ya wanawake na vijana kwa kuwa ilionekana Shirika la Rafiki limewapelekea vyerehani vitano lakini vitatu tayari havipo",alisema Azza.

Hata hivyo hoja ya kuwapatia mikopo ilipingwa na madiwani ambao walisema sehemu kubwa ya wakazi wa Mwakitolyo ni watu wanaotoka maeneo ya nje ya wilaya ya Shinyanga ambao wamekwenda pale kufanya biashara ya madini na hawana anuani maalumu.

Baada ya mjadala mrefu, madiwani hao walimuagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuchukua hatua za haraka za kudhibiti vitendo hivyo na pia kuwaomba madiwani wa viti maalumu kwenda kutoa elimu  kwa wanawake wenzao wanaofanya vitendo hivyo kwa kuwaeleza madhara wanayoweza kuyapata.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Mboje Ngassa aliagiza kazi ya kwenda kutoa elimu kwa watu wanaofanya biashara hiyo ifanyike mapema wiki ijayo ambapo amemuomba mbunge wa viti maalumu, Azza Hilal ashirikiane na madiwani wa viti maalum katika suala hilo.

“Ni vitendo vinavyosikitisha, inaonesha ni ukosefu wa elimu kwa wenzetu hawa walioamua kujitoa ufahamu, hawajui madhara ya kile wanachokifanya, sasa tukawaelimisha, nafikiri wataacha, kwa suala la mikopo, litakuwa gumu kidogo maana wengi wao si wakazi wa wilaya ya yetu,” alieleza Ngassa.
Mwisho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com