Na Mwandishi Wetu Mbeya
Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NGOs) Bi. Vickness Mayao ameyaondoa Mashirika zaidi ya 158 kwenye Rejista ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Hayo yamesema jijini Mbeya na Mkurugenzi Msaidizi Uratibu wa NGOs kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi Grace Mbwilo kwa niaba ya Mkurugenzi na Msajili wa NGOs nchini.
Bi. Grace amesema kuwa katika Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Namba 24 ya Mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa Mabadiliko na Sheria Namba 3 ya Mwaka 2019, imefafanua bayana kuwa jukumu la kusajili mashirika yanayoendesha shughuli za kijamii, kiutamaduni, kiuchumi, utawala bora, haki za kibinadamu na mazingira katika ngazi ya jamii kwa lengo la kutogawana faida na ambazo hazina mrengo wa wa kukuza biashara, zimeelekezwa kusajililiwa na Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs).
“Mashirika yaliyoondolewa kwenye daftari la Msajili wa NGOs ni yale ambayo yalisajiliwa chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 ambayo yanafanya kazi kwa lengo la kunufaisha wanachama wake, kugawana faida, yenye mlengo wa dini, yenye lengo la kukuza biashara na Bodi za wadhamini”, alisema Bi. Grace.
Bi. Grace ameongeza kuwa, hatua ya kuyaondoa mashirika haya kwenye daftari la msajili wa NGOs imefikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Marekebisho Na. 3 ya mwaka 2019 iliyoanza kutekelezwa kuanzia tarehe 1 Julai 2019. Kwa mujibu wa Sheria, Mashirika hayo yanatakiwa kwenda kujisajili chini ya Sheria husika ikiwemo Sheria ya Jumuiya za Kijamii(Sura ya 337), Sheria ya Munganisho wa Wadhamini(Sura ya 318) na Sheria ya Makampuni (Sura ya 212), na kwamba inatakiwa kukamilisha zoezi hili kabla ya tarehe 01 Septemba,2019.
Ameeleza kuwa wa kuzingatia ufafanuzi wa mipaka ya usajili ulioainishwa na Sheria Namba 3 ya Mwaka 2019, Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) anayakumbusha Mashirika yanaofanya shughuli kwa lengo la kugawana faida, yenye mrengo wa dini na ambayo yana malengo wa kukuza biashara, kwamba mashirika ya aina hiyo yatafutwa kwenye daftari la Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali baada ya kipindi cha miezi miwili kuanzia tarehe 01.07.2019 na yatahamishiwa chini ya Mamlaka nyingine za Usajili kutokana na kukosa sifakuwa NGO.
Katika kuhitimisha zoezi la usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali liliofanyika Mkoani Mbeya, Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali imewaagiza wadau wa mashirika yote yaliyosajiliwa kwa lengo la kuzalisha faida na kugawana faida kuhakikisha kuwa wanahamisha usajili ili kuhuisha taarifa zao kwa Msajili stahiki.
Hatua hii imechukuliwa na Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika hatua ya mwisho ya Usajili wa Mashirika hayo kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayohitimishwa mwisho wiki katika ukumbi wa Mkapa Jijini Mbeya na orodha ya Mashirika 158 yaliyoondolewa kwenye daftari inapatikana katika tovuti ya Wizara www.mcdgc.go.tz na ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. www.tnnc.go.tz
Social Plugin